Rais wa Klabu Bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Joan Laporta amesisitiza kwamba Mshambuliaji Ansu Fati hatauzwa katika dirisha hili la usajili ambalo litafikia tamati Septemba 31.
Winga huyo alitajwa sana kwamba ana mpango wa kuondoka FC Barcelona huku akihusishwa na Wolverhampton Wanderers mapema dirisha la usajili la kiangazi lilipofunguliwa.
Lakini, Rais huyo aliweka wazi wikiendi iliyopita kwamba Fati ni mchezaji muhimu katika timu hiyo na kila mtu anampenda.
“Niuamuzi wa Xavi (kocha Hernández) ndio maana alimjumuisha katika kikosi. Ni mchezaji mzuri katika timu na tunachotaka ni kuimarika zaidi. Tuna furaha sana kwa sababu bado yupo na sisi,” alisema Laporta.
Awali, FC Barcelona ilikuwa na nia ya kumuuza Fati na baba yake mzazi aliwahi kuja juu akidai klabu hiyo haimpi heshima anayostahili mwanaye.
Ishu ya Fati inafanana na sekeseke la usajili wa Frankie de Jong ambaye alikuwa mbioni kuuzwa dirisha la usajili la kiangazi mwaka jana, lakini uhamisho wake ulikwama.
Manchester United ilionyesha nia ya kumsajili De Jong, wakati FC Barcelona ikionyesha nia ya kumuuza kwa lengo la kujipatia fedha za usajili kwa sababu ilikuwa ikikabiliwa na janga la kiuchumi.
Mdachi huyo aliweka mkazo kwamba hana mpango wa kuondoka licha ya klabu hizo kufikia makubaliano juu ya ada ya uhamisho taarifa iliyotolewa na mkali wa masuala usajili, Fabrizio Romano.
Kocha wake wa zamani aliyemnoa Ajax, Erik ten Hag licha ya kupambania uhamisho huo hakufanikiwa badala yake aliishia kumsajili Casemiro kwa Pauni 70 milioni kutoka Real Madrid.
Fati alianza kujulikana alipofunga bao akiwa na umri wa miaka l6 mwaka 2019 na tangu hapo alikabidhiwa jezi namba 10 iliyovaliwa na Lionel Messi.