Rais wa Klabu Bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Joan Laporta amewashangaa mastaa wenye majina makubwa ambao wameamua kuondoka Ulaya na kufuata pesa za Waarabu.
Ronaldo ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza wa Ulaya kuhamia huko akiwa na klabu ya Al-Nassr na alijiunga kipindi cha usajili wa kingazi lililopita. Lakini Laporta anaamini mastaa hao wamehamia huko kutokana na sababu ambazo sio sahihi kwenye soka.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha CNN, alisema: “Wakati mchezaji mkubwa mwenye heshima anapohamia Saudi Arabia kuna sababu nyingi na sio michezo, sijaona sabababu yoyote, ninachoamini soka ndio jambo ambalo linatakiwa kupewa kipaumbele na kwenye hilo sijaona kitu.”
Hivi karibuni Jordan Henderson, Fabinho, Riyad Mahrez na Sadio Mane nao wamefuata nyayo za mastaaa wengine waliotimikia Saudi Arabia na watakuwa wakilipwa pesa defu.
Pia, iliripotiwa hivi karibuni Al-Hilal ilitoa ofa iliyoweka rekodi ya dunia kwajili ya Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe ambayo ilitajwa kuwa ni Pauni 259 milioni- hata hivyo, nyota huyo aligoma kuzungumza na uongozi wa klabu hiyo.
Kauli ya Laporta inakuja baada ya Pep Guardiola kusema klabu za Ligi Kuu England zisipuuzie kwa sababu Saudi Arabia itakuwa tishio zaidi siku za usoni baada ya kushindwa kumzuia Mahrez asimtimkie huko.
Kwa mujibu wa Guardiola alikuwa hana nia ya kumuuza Mahrez kwenda Al-Hilal lakini kutokana na nguvu ya pesa za Waarabu alishindwa kumshawishi abaki Etihad.