Klabu ya Man City imefikia pazuri katika mipango ya kumsajili mlinda mlinda mlango wa klabu ya Benfica Ederson Moraes, baada ya mazungumzo ya viongozi wa pande zote mbili kwenda sawa.
Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23 amekua katika mipango ya Pep Guardiola kwa kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita, na huenda akawa mchezaji wa kwanza kutua Etihad Stadium mwishoni mwa msimu huu.
Matarajio ya usajili wa Mbrazil huyo yanadhihirisha huenda walinda mlango wa Man City waliopo kikosini kwa sasa Claudio Bravo na Willy Caballero wakapata wakati mgumu wa kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza.
Mbali na matarajio hayo, kwa upande wa mlinda mlango Joe Hart aliepelekwa kwa mkopo nchini Italia kwenye klabu ya Torino, atakua amefutiwa ndoto zake za kurejea klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa kutoka nchini Ureno ambazo zimechukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari mapema hii leo, zinaeleza kuwa, viongozi wa Man city wameafiki kumsajili mlinda mlango huyo, huku thamani yake ikitajwa kufikia paundi milioni 30.