Kocha Mkuu wa Taifa Stars kim Poulsen ameeleza masikitiko yake baada ya kumkosa Nahodha na Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC John Bocco, kwenye kikosi chake ambacho jana kiliibanjua Madagascar mabao 3-2, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Stars iliibuka na Ushindi katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika nchini Qatar huku mabao yakifungwa na Erasto Nyoni, Feisal Salum na Novatus Dismas.
Kocha Kim amesema alikuwa na wakati mgumu wa kuchagua wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji kwa sababu timu nyingi za Tanzania zinasajili wachezaji wa kigeni, huku akionesha furaha yake juu ya Reliant Lusajo kwa kuonesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa jana Jumanne (Septamba 07) akihudumu katika nafasi hiyo.
Baada ya ushindi huo Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo chini ya waziri wenye dhamana Innocent Bashungwa, amesema kuwa kikosi cha Taifa Stars kitapokea kitita cha Tshs. Million 10 kama motisha kwa kwachezaji.
”Kwa matarajio yangu, kwa sababu tumejizatiti wakiwa kambini wafanye mazoezi vizuri wakiwa na walimu wazuri pia natoa wito kwa benchi la ufundi kuendelea na moyo huo huo, na kwafuraha niliyonayo kwaniaba ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, tutawaandalia Tshs. Million 10. kama sehemu ya motisha.”
Kwa upande wa mchezaji wa Taifa stars Saimon Msuva amesema kuwa michuano ya kufuzu fainali za kombe la dunia ni migumu na kila timu imejizatiti kufanya vizuri na zenye wa wachezaji wanaocheza ligi za Ulaya, akisisitiza kuwa timu itakayojipanga vizuri ndiyo yenye nafasi ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Ushindi wa mabao 3-2 unaiwezesha Taifa Stars kuongoza msimamo wa kundi J, lenye timu za Benin, DR Congo na Madagascar.
Taifa Stars imefikisha alama 4 sawa na Benin baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya DR Congo uliomalizika kwa sare ya 1-1 na Madagascar uliomalizika kwa ushindi wa mabao 3-2.