Tovuti ya 90minutes imeripoti Beki wa kushoto kutoka nchini Hispania Jordi Alba, atajiunga na Inter Miami kwa uhamisho wa bure, akiungana na wachezaji wenzake wa zamani wa FC Barcelona, Lionel Messi na Sergio Busquets.
Timu hiyo ya Ligi Kuu ya soka ya Marekani, ilianza kumfuatilia beki huyo majuma kadhaa yaliyopita, baada ya Alba kuthibitisha kuondoka FC Barcelona kutokana na kumalizika kwa mkataba wake.
Anaondoka FC Barcelona akiwa amecheza mechi 459 kwa jina lake katika kipindi cha miaka 11.
Ndiye mchezaji wa hivi karibuni atakayesajiliwa Inter Miami, ambao wameamua kurekebisha orodha yao wakati wa dirisha la uhamisho.
Kwa mara ya kwanza walimtangaza Lionel Messi mnamo Juni 7, baada ya mchezaji huyo kufichua dhamira yake ya kuichezea timu hiyo.
“Nilifanya uamuzi kwamba nitaenda Miami,” amesema Messi.
Inter Miami walithibitisha kuwasili kwa Sergio Busquets majuma machache baadaye, kabla ya kumtangaza Gerardo ‘Tata’ Martino kuwa kocha mkuu wao mpya zaidi.
Watatu hao walicheza pamoja katika Ligi Kuu Hispania, La Liga, kuanzia mwaka 2012 hadi 2021, wakishinda mataji matano ya ligi, sita ya Copa del Rey na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.