Mmiliki wa Klabu ya Inter Miami CF, Jorge Mas, amesema ilimchukua miaka mitatu ya mazungumzo kumsajili Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Soka Marekani, MLS.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2022, akiwa na Argentina, Messi alitangaza mwezi uliopita kuwa atajiunga na Inter Miami kama mchezaji huru baada ya misimu miwili kule Paris Saint-Germain.

“Mwaka 2019 wakati Messi akiwa bado Barcelona, tulianza kufikiria jinsi ya kumleta,” amesema Mas akiliambia gazeti la Hispania la El Pais.

“Nilitumia miaka mitatu kulishughulikia hili, mwaka mmoja na nusu nikifanya kazi kwa bidii sana. Kulikuwa na mazungumzo mengi na baba yake Messi ambaye ni wakala wake, Jorge.

“Mmiliki mwenzangu wa Inter Miami, David Beckham, alizungumza na Leo kuhusu masuala ya soka tu, kwa sababu alikuwa mchezaji.”

Messi mwenye umri wa miaka 36, awali alikuwa amefikiria kurejea Barca, klabu ambayo aliiacha mwaka 2021 kutokana na matatizo yake ya kifedha, huku pia akikataa mkataba mnono kutoka Saudi Arabia.

“Niliona kama imefanywa mwishoni mwa Mei,” Mas amesema.

“Sikutaka ajisikie chini ya shinikizo. Tulikuwa tumezungumza kule Barcelona, Miami, Rosario, Doha nilitumia Kombe zima la Dunia kule Qatar, nikiitazama Argentina.

“Mkataba wa Apple ulikuwa muhimu sana kufunga mpango huo.”

Messi, ambaye yuko likizo, anatarajiwa kusaini mkataba na Inter Miami hadi Desemba 2025, na chaguo la kuongeza mwaka mmoja, wakati Mas alithibitisha kuwa fowadi huyo atalipwa kati ya Pauni milioni 50 na 60 kwa mwaka.

Mas pia amethibitisha nia ya muda mrefu ya kumzunguka Messi na wachezaji anaowafahamu, wakiwamo Sergio Busquets na Jordi Alba.

Pia amesema Miami itasajili wachezaji “wawili au watatu” zaidi lakini akapuuza ripoti kwamba marafiki wawili wa karibu wa Messi, fowadi wa zamani wa Barca, Luis Suarez na winga wa Argentina, Angel Di Maria wanaweza kuwasili msimu huu wa majira ya joto.

Jibril Sillah: Azam FC ni mahala sahihi kwangu
Balozi Kayola awasilisha hati za utambulisho Malawi