Kocha Mkuu wa AS Roma, Jose Mourinho huenda akaondoka 2024, kwa mujibu wa ripoti kutoka Italia.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United alijiunga na AS Roma 2021 na kuiongoza kubeba ubingwa wa Europa Conference League msimu wake wa kwanza.
Pia aliiongoza kutinga fainali ya Europa msimu uliopita, lakini ameanza vibaya msimu huu na anajiandaa kumenyana na Inter Milan kwenye mechi ya Serie A kesho Jumapili (Oktoba 29).
Mourinho mwenye umri wa miaka 60, bado ana mkataba na AS Roma utakaomalizika mwakani na inasemakana hana mpango wa kubaki baada ya hapo.
Kwa mujibu wa TeamTalk Mourinho yupo mbioni kuondoka baada ya mkataba kumalizika na hiyo inamaanisha AS Roma itaanza maisha mapya bila ya kocha huyo.
Pia imeripotiwa wachezaji kadhaa wataondoka akiwemo staa wa zamani wa Chelsea, Tammy Abraham mwenye umri wa miaka 26.
Mshambuliaji huyo alikuwa usajili wa kwanza wa Mourinho na amefunga mabao 25 katika mechi 75 za Serie A tangu alipotua kikosini akitokea Chelsea alikoonekana kama garasa kwa wababe hao wa Darajani.
Wakati huohuo AS Roma inaamini itamchukua jumla Mshambuliaji Romelu Lukaku anayekipiga kwa mkopo kutoka Chelsea utakapomalizika itakapofika wakati wa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mwakani.
Pia Abralham atafungua njia kuhusishwa katika dili hilo ili kurejea Chelsea katika klabu yake ya utotoni.
Kwa mujibu wa ripoti Chelsea inafuatilia mwenendo wake tangu ilipomuuza ingawa itapata ushindani kutoka kwa wapinzani.