Meneja wa AS Roma ya Italia Jose Mourinho anaripotiwa kuwa katika mipango ya kulamba dili la pesa nyingi kutoka Saudi Arabia.
Meneja huyo kutoka nchini Ureno amebakiza miezi 12 tu katika mkataba wake wa sasa huko katika klabu ya AS Roma.
Kumekuwa na uvumi kwamba anafikiria mpango wa kuondoka kwenye majira haya ya kiangazi huko Ulaya baada ya AS Roma kushindwa kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu yote miwili aliyokuwa akiinoa timu hiyo.
Kwa mujibu wa Foot Mercato, klabu ya Al-Hilal imemworodhesha Mourinho kuwa chaguo lao la kwanza kwenye msako wa kocha mpya na kwamba wameandaa ofa nono kabisa ili akapige kazi huko Mashariki ya Kati.
Na kinachoelezwa ni kwamba Mourinho mwenye umri wa miaka 60, atapewa mkwanja mrefu wa kusajili.
Roma wanataka kumbakiza Mourinho, lakini wamefungua milango ya kuachana na kocha huyo na kutafuta mwingine wa kuja kuchukua mikoba yake.
Ligi Kuu Saudi Arabia, Saudi Pro League ipo bize kwa sasa kuvuta mastaa wenye majina makubwa kwenye soka kwenda kwenye ligi hiyo.
Cristiano Ronaldo alifungua milango kwa kujiunga na Al-Nassr, wakati fowadi mwingine wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema naye amejiunga na Al-Ittihad. Kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga na Al-Ittihad huku Al-Ahli wakihitaji pia saini ya mkali wa Manchester City, Riyad Mahrez.
Taarifa nyingine za kutoka Saudi Arabia, zinadai kwamba Al-Hilal inayomtaka Mourinho, inamtaka pia Neymar.