Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa neno lingine ambalo ni kati ya makosa yaliyokuwa yanafanywa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alipofanya kazi na jeshi la polisi.
Akizungumza leo, Januari 27, 2020 baada ya kumuapisha George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alimtaka kuwa mwangalifu na kuzingatia taratibu za kijeshi anapofanya kazi na jeshi.
Alisema maamuzi yasiyozingatia sheria yaiyofanywa na watangulizi wake katika wizara hiyo dhidi ya askari yalisababisha Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro kulalamika kwake.
Rais Magufuli alisema kuwa kufuata utaratibu na kuwaheshimu viongozi wa Jeshi ni moja kati ya sababu zinazomfanya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi kuendelea kudumu kwenye wizara hiyo.
“Umesema hapa kwamba wewe huna nyota hata moja… hivi vyombo vya ulinzi na usalama vina namna yake ya kuviendesha, ndio maana Waziri Mwinyi amekaa sana Wizara ya Ulinzi; hawezi akasimama hapo mbele akawatukana mabrigedia hawa, anajua namna ya ku-operate,” alisema Rais Magufuli.
“Na ndio maana unaona wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaripoti moja kwa moja kwa Rais. Sasa ukishapima hizo inaweza ikakusaidia sana namna yak u-operate. Mimi najua wewe ni mwanasheria na ndio maana ulivyoanza hapa niliona IGP anatingisha kichwa, nafikiri amefurahi sana; kwa sababu saa zingine alikuwa anakuja kwangu analalamika anasema ‘nimeshaambiwa hawa niwatoe, lakini Order [Standing Order] haisemi hivyo’. Nikamwambia ‘bana nenda ukawatoe’. Lakini kwakweli saa nyingine sio utaratibu,” aliongeza.
Mkuu huyo wa nchi pia aligusia barua aliyoandikiwa na Waziri Lugola akimuomba kupitisha utaratibu wa kuingia mkataba aliouita wa ‘hovyo’ kati ya Jeshi la zima moto na Uokoaji na kampuni moja ya nchini Romania. Alieleza kukasirishwa na hatua hiyo kwani hakuwa anafahamu chochote kuhusu mkataba huo.
Rais alitengua uteuzi wa Lugola, alipokuwa akizindua nyumba za askari wa jeshi la magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam. Alisema kuwa ingawa anampenda lakini hataweza kuvumilia jinsi wizara hiyo ilivyokubali kuingia mkataba wa hovyo, ikiwa ni pamoja na kuomba mkopo nje ya nchi bila kufuata taratibu za nchi. Thamani ya mkataba huo ni zaidi ya Sh 1.2 trilioni.
Leo, Magufuli alimueleza Simbachawene kuwa amempeleka kwenye Wizara ngumu ambayo amesema ni ‘kama ina mapepo’. Hivyo, amemtaka amtangulize Mungu ili aweze kufanikisha kuiweka sawa kwani kuna mambo mengi ya hovyo yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo. Alisema ingawa amekuwa akiwatahadharisha mawaziri wote wanaoingia kwenye wizara hiyo, bado walishindwa kufaulu mtihani huo.
Akizungumza awali, Waziri Simbachawene aliahidi kufanya kazi kwa kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama ili viweze kufanya kazi yake na yeye atafanya kazi yake ya kiutawala
“Mahala ambapo ni pa kiutawala tutakwenda kiutawala, lakini Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii ni wewe, mimi sichangii na wewe nafasi hiyo, nitaviheshimu vyombo viweze kufanya kazi yake na mimi nitafanya kazi za kiutawala. Pale ambapo vyombo vinafanya makosa kazi yangu mimi ni kukutaarifu kwamba kuna mambo hayako sawa, lakini mimi sina cheo chochote na sina nyota yoyote na haukunipa nyota leo hapa,” alisema Simbachawene.