Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli leo Septemba 27, 2018 amefanya uzinduzi wa barabara ya juu (Flyover) Tazara iliyopewa jina la Mfugale Flyover.

Rais, JPM amesema ameridhia barabara hiyo kuitwa jina hilo kutokana kwamba, Mhandisi Patrick Mfugale amefanya kazi nyingi hapa Tanzania hali ambayo imeonesha uzalendo mkubwa.

Takwimu zake zinasoma kwamba mpaka sasa Mhandisi Mfugale amejenga barabara zaidi ya elfu moja hapa nchini.

”Kwa kazi ambazo amekuwa akizifanya tangu akiwa mhandisi kuanzia mwaka 1977 alipokuwa  Wizara ya Ujenzi ninaamini kabisa ndugu zangu watanzania  mtakubaliana na mimi kwamba flyover hii kwa kazi kubwa alizozitaja alizozifanya injinia Mfugale ilistahili kuitwa Mfugale Flyover” amesema Magufuli wakati akihutubia wananchi kwenye uzinduzi huo.

Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa wataalamu wote hapa nchini kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale wa kuchapa kazi na kuweka pembeni ubinafsi ambao mwisho wa siku huleta majanga kwa taifa.

”Nitoe wito kwa wataalamau wetu hapa nchini waige mfano wa uchapa kazi wa Mfugale, Mfugale hakupendelewa ni haki yake yapo mengi aliyoyafanya kwa nchi ametanguliza Utanzania badala ya kutanguliza ubinafsi, wapo wataalamu wetu wachache ambao kwa sababu zao wenyewe wanazozijua wamekuwa chanzo cha matatizo hapa nchini” ameongezea Rais Magufuli.

 

Carlo Ancelotti hajui nani ataikabili Juventus
Unai Emery akanusha kuzuia mpango wa Joachim Low