Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli, ameagiza kujengwa kituo kikubwa cha kupaki magari na kituo cha daladala ili kuwawezesha wananchi wanaotumia magari binafsi kupaki Kimara mwisho na kutumia usafiri wa mwendokasi ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es salaam.
Ameyasema hayo mapema hii leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji wa Huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika Kituo Kikuu cha Mabasi kilichopo Kariakoo eneo la Gerezani.
“Wito wangu ni kwamba kuna watu wengi wana magari madogo madogo na wanatoka sehemu mbalimbali mpaka kufika kituo cha Kimara mwisho na kuna eneo kubwa pale la hifadhi ya barabara ambalo halihitaji hata kulipa fidia ili kulitumia,wananchi wanaona adha ya foleni iliyopo lakini hawana sehemu ya kupaki magari yao ili watumie magari ya mwendo kasi,nawaomba mjenge kituo cha magari madogo madogo eneo hili la Kimara ili wananchi hawa wafaidike vyema na mradi huu”, aesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kujengwa kwa kituo cha mabasi ya daladala katika eneo la Kimara mwisho ili kuwasaidia wananchi wanaofika katika kituo cha magari ya mwendokasi kutopata shida ya kuunganisha magari ya kwenda Mbezi na sehemu nyingine za Jiji kwani watakuwa na kituo rasmi.
Awali akizungumzia mradi huo Rais Magufuli alisema kuwa iliwachukua abiria kusafiri kwa zaidi ya masaa matatu kutoka Kimara mpaka posta lakini kukamilika kwa mradi huu kumesaidia kurahisisha abiria kufika kituo cha Posta kwa kutumia dakika 30 mpaka 40 na hivyo mradi huu kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu wa awamu ya kwanza wenye kilometa 20.9 umetumia jumla ya shilingi bilioni 403.5 ambapo Tanzania imechangia bilioni 86.5 na Benki ya Dunia wametukopesha bilioni 317.
Hata hivyo, Rais Magufuli ametoa shukrani kwa Benki ya Dunia kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha mradi huu na miradi mingine nchini na kuwataka kusaidia katika kufanikisha mradi wa kujengwa kwa barabara za juu katika eneo la Ubungo na wale wote wanaohusika katika kupata mkandarasi wafanikishe haraka suala hilo ili kusaidia mabasi yaendayo haraka kupita kwa urahisi na hivyo kutimiza dhana halisi ya mabasi hayo