Kocha Juan Antonio Pizzi anatarajia kujiuzulu kuinoa timu ya taifa ya Chile, baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia kupitia ukanda wa kusini mwa Amerika.
Timu ya taifa ya Chile (La Roja), ilikubali kupoteza mchezo wa leo alfrajiri kwa kufungwa mabao matatu kwa sifuri na Brazil mjini Sao Paulo, na kujikuta wakiporomoka hadi kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wa kundi la ukanda wa kusini mwa Amerika.
Matokeo ya sare ya bao moja kwa moja kati ya Peru na Colombia, pia yamechangia kufeli kwa timu ya taifa ya Chile kufikia lengo la kucheza fainali za kombe la dunia za 2018, zitakazounguruma nchini Urusi.
Kwa matokeo hayo ya sare, Peru wameshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi, na sasa watacheza mchezo wa mtoano dhidi ya mshindi kutoka ukanda wa Oceania (New Zealand).
Juan Antonio Pizzi alionyesha kuwa tayari kujizulu nafasi yake, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mchezo dhidi ya Brazil kumalizika, kwa kusema hana budi kuheshimu maamuzi aliyoyatangaza juma lililopita.
“Niliahidi mbele yanu juma lililopita, nilisema kushindwa kwa Chile katika harakati za kombe la dunia 2018 kutanifanya nisitishe mkataba wangu.
“Nina kila sababu ya kufanya hivyo ili kulinda heshima yangu, na kuwaachia wengine kujaribu bahati yao kama watafanikiwa, nimejitahidi kadri nilivyoweza lakini hatukufanikiwa kama tulivyokusudia.
“Saa kadhaa ama siku chache zijazo, mtakua na taarifa mpya kunihusu.” Alisema Pizzi.
Timu ambazo tayari zimeshafuzu fainali za kombe la dunia 2018 kutoka ukanda wa kusini mwa Amerika ni Brazil, Colombia, Argentina na Uruguay.