Kocha Msaidizi wa Manchester City, Juanma Lillo amesisitiza timu hiyo ipo katika ubora licha ya Pep Guardiola kutokuwepo kutokana na maradhi ya mgongo yanayomsumbua.
Lillo alirejea Etihad mwezi huu baada ya kuitema Al-Sadd kutoka Qatar na ataiongoza Man City mpaka Guardiola atakapopata nafuu baada ya opereshi ya mgongo aliyofanyiwa juma lililopita.
Sasa mashabiki wamepata hofu kama kocha huyo msaidizi ataweza kuiongoza Man City kipindi hiki ambacho Guardiola hayupo kikosini.
Kwa mujibu wa taarifa Guardiola atarejea katika majukumu yake baada ya mechi za kimataifa lakini kocha huyo msaidizi akawaondoa hofu mashabiki akidai timu ipo mikono salama.
“Wote tunajaribu kuvaa kiatu cha Guardiola, itasaidia timu kuimarika zaidi, Tulifanya kazi pamoja kwa muda mrefu, tulikuwa marafiki wa karibu na tunaelewa vitu kwani mawazo yetu yanafanana, siku zote anapenda kuimarika na kuvumbua vitu vipya,” alisema Lillo.
Guardiola alimsifia Lillo kutokana na utaalamu wake wa soka ndio maana anaamini uwezo wake wa kufanya kazi kwa sababu ana uzoefu pia.
Lillo ni mmoja wa kocha mwenye uzoefu ambaye amedumu katika soka kwa muda wa miaka 22 na alifundisha soka katika mabara manne.
Guardiola na Lillo walianza ufariki tangu walipokuwa wanacheza soka mwaka 2005 katika klabu ya Dorados Sinaloa kutoka Mexico.