Kiungo Jude Bellingham amesema anataka kubakia Real Madrid kwa miaka 10 hadi 15 ijayo baada ya kudai timu hiyo ya Ligi Kuu Hispania (La Liga), imesaidia kukipaisha kipaji chake katika kiwango kipya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alicheza nafasi kubwa katika ushindi wa mabao 3-1 wa England dhidi ya Italia kwenye Uwanja wa Wembley hapo mapema juma hili akiwasaidia The Three Lions kupata nafuu baada ya bao la kwanza la Gianluca Scamacca dakika ya 15 na kufanikiwa kupata ushindi ambao uliwafanya wafuzu Euro 2024.
Kane aliongeza bao la tatu la dakika za mwisho na kuipa England ushindi wa kwanza dhidi ya Italia katika ardhi ya nyumbani tangu 1977, na kulipiza kisasi kwa kushindwa kwao fainali ya Euro 2020 na wapinzani wao hao miaka miwili iliyopita.
Bellingham sasa ana mabao 11 na asisti sita katika mechi 13 za klabu na nchi msimu huu kufuatia uhamisho wake wa majira ya joto kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya awali ya euro milioni 103.
Jude Bellingham aliiambia Channel 4: “Ninaimarika kidogo kila ninapocheza. Ulikuwa usiku mzuri sana kwetu, sote tunakumbuka kilichotokea miaka michache iliyopita walipocheza hapa. Siku zote unalenga maendeleo. Sisi kuelekea katika mwelekeo sahihi na ushindi muhimu sana kwetu.
“Napenda soka kwa sasa. Uongozi wangu katika klabu na nchi unanipa uhuru wa kuucheza jinsi ninavyotaka.
“Tangu miezi michache iliyopita nimekuwa nikifanyia kazi muda wangu wa kuingia kwenye boksi na ninapowasili nawasili na njaa kali.
“Pamoja na uhamisho mkubwa ukweli ni kwamba ni lazima nifanye, iwe ni bao au pasi ya mabao au ushindi wa mechi.
“Hii ndiyo klabu ninayotaka kuwa nayo kwa miaka 10 hadi maisha yangu.”