Kiungo kutoka nchini England Jude Bellingham amesifu ushirikiano wake na Vinícius Jr akimwita mshambuliaji huyo bora zaidi duniani baada ya wawili hao kuwa kwenye ukurasa wa mabao katika ushindi wa 3-2 wa Real Madrid kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya SSC Napoli.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alitoa pasi kwa Vinicius aliyefunga bao la kusawazisha baada ya Leo Ostigard kuwaweka wenyeji mbele kwenye Uwanja wa Diego Armando Maradona, na Bellingham akaiweka Madrid mbele kwa mabao 2-1 kabla ya muda wa mapumziko.
Piotr Zielinski alifanya mambo kuwa 2-2 kwa penalti kabla ya Federico Valverde kupiga shuti lililompita kipa, Alex Meret na kutinga wavuni na kuipa Madrid pointi zote tatu, na kuwaacha kileleni katika Kundi C.
“Pengine ndiye bora zaidi duniani kwa upande kwangu,” alisema Bellingham akiiambia Movistar, alipoulizwa kuhusu ushirikiano wake na Vinicius.
“Yeye ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji zaidi ambao nimewahi kucheza nao.
Bellingham sasa amefunga mabao nane katika mechi tisa za kwanza akiwa na Real Madrid katika mashindano yote.
“Ninajiamini, lakini sikujua itakuwa nzuri hivi,” alisema.
“Nina deni kwa wafanyakazi na wachezaji wenzangu.”
Bao la Bellingham ambalo lilimuona kiungo huyo akiuchukua mpira ndani ya nusu ya wapinzani kabla ya kuanza kukimbia pekee yake lililinganisha lile na nguli wa zamani wa SSC Napoli na Argentina, Maradona.