Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kupewa pongezi kwa juhudi zake endelevu za kuifungua nchi kiuchumi, ambazo zimechangia Diplomasia ya Mikutano nchini kuendelea kustawi kwa kasi hatua ambayo inachangia kuimarisha shughuli za kiuchumi na kukuza pato la Taifa.
Pongezi hizo, zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha – AICC, Ephraim Mafuru hii leo Septemba 14, 2023 wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini ikiwa ni mwendelezo wa vikao kazi baina ya taasisi na mashirika ya umma chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, “kwa sasa, wageni wanaipenda Tanzania na wanakuja Tanzania kwa wingi, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kazi kubwa ya kufungua nchi kuna Royal Tour, lakini amekuwa akishiriki mikutano mbalimbali kuitangaza nchi, hivyo Tanzania imeendelea kuwa chaguo muhimu na kuvutia mikutano mbalimbali ya Kimataifa.”
Mafuru ameongeza kuwa, baada ya kampeni kubwa ya kufungua nchi,wamekuwa na asilimia 10 ya market shares katika Afrika, hivyo kwa sasa wanandaa mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafikia malengo makubwa ya kuleta kwa wingi fedha za kigeni nchini.