Jukwaa la katiba Tanzania (Jukata), kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat) Dk Lugelemeleza Nshala watafungua kesi kupinga katazo la maandamano wakati wowote kuanzia sasa.

Hayo yameongelewa jana na Mkurugenzi wa Jukata, Hebron Mwakagenda, akidai kuwa wanaushahidi wa kutosha kusimamia kesi hiyo.

“Kikubwa katika mwaka huu ni kufungua kesi ya kupinga katazo la maandamano, maana ni kama yamefutwa kiaina hivi’’. amesema Hebron Mwakagenda.

Aidha amesema kuwa “Tumekusanya ushahidi wa kutosha, ukiwemo wa sisi wenyewe. tuliomba kufanya maandamano Polisi tukakataliwa kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu. Tukaomba tena tukakataliwa, huo ni sehemu ya ushahidi wetu.”

Katazo la shughuli za siasa lilianza kutolewa na Jeshi la Polisi Novemba 6, 2015 likipiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwa madai ya kuwapo hali tete ya kisiasa.

Januari 23, 2016, Rais John Magufuli mwenyewe alitangaza kusimamisha shughuli za siasa ikiwa pamoja na mikutano na maandamano, alipokuwa akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakati huo, Jaji Damian Lubuva.

 

Mamlaka ya hali ya hewa yatoa angalizo
Benki kuu ya Tanzania yazifutia leseni benki tano