Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes Jamhuri Kihwelo Julio, amesema licha ya kuondoshwa kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 20 (AFCON 20) vijana wake wamejifunza vitu vingi vitakavyowasaidia siku za usoni.
Tanzania ‘Ngorongoro Heroes’ ilitupwa nje ya fainali hizo rasmi jana Jumatatu, baada ya kufungwa na Morocco mabao matatu kwa sifuri, na kumaliza ikiwa mkiani mwa ‘KUNDI C’ kwa kumiliki alama moja.
Kocha Julio amesema kwa hakika michuano hiyo imekua funzo kubwa kwa wachezaji wake, na imewapa kitu cha kujifunza katika maisha yao ya soka kwa siku za usoni.
Amesema hata yeye kama kocha mkuu wa ‘Ngorongoro Heroes’ amejifunza mambo mengi kutoka kwa makocha wenzake, na ameahidi kuyatumia kwa maslahi ya soka la Tanzania ambalo kwa sasa linawatazama sana vijana.
Julio ameongeza kuwa kila timu katika michuano hiyo imejipanga na hata wao walijipanga lakini bahati haijawa upande wa Tanzania.
“Mashindano ni mazuri, tumepoteza ni sehemu ya mchezo ila nina imani vijana wangu wamepata vitu ambavyo vitatusaidia siku za usoni,”
“Tuecheza na timu zenye uzoefu mkubwa katika michuano hii, japo tulionesha kupambana, lakini bahati haikuwa kwetu, hata mimi kama kocha nimejifunza baadhi ya mambo kutoka kwa wenzangu na nitayatumia kwa maslahi ya soka la vijana.’ Amesema Julio.
Kabla ya kufungwa na Morocco jana Jumatatu, Tanzania ‘Ngorongoro Heroes’ ililazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Gambia, huku ikipoteza dhidi ya Ghana kwenye mchezo wa ufunguzi wa ‘KUNDI C’.