Aliyewahi kuwa Mchezaji na Kocha Simba SC Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amefichua baadhi ya mambo ambayo anaamini huenda yakawa chanzo cha kuikwamisha timu hiyo kuonesha soka safi, licha ya kuibuka na ushindi katika michezo mitatu ya Ligi Kuu na kuambulia sare dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Julio amesema licha ya kikosi hicho kushindwa kupata muunganiko mpaka sasa kocha Robertinho anatakiwa kuendelea kuwarudishia ubora wachezaji wake pamoja na kucheza kwa nidhamu.
Akitolea mfano katika mchezo uliopita dhidi ya Power Dynamos, Kocha huyo amesema kulikuwa na makosa makubwa kwenye mchezo huo uliounguruma Azam Complex, Chamazi yanayotokana na kiwango kidogo cha uwajibikaji.
“Simba SC bado haijapata muunganiko, Simba SC ilikuwa inacheza vizuri na inafunga mabao lakini bado ubora huo msimu huu hawajaweza kuupata na mashabiki wanakitaka hicho hasa wakiwaangalia wapinzani wao Young Africans wanafanya vizuri,” amesema Julio ambaye alikuwa akicheza nafasi ya beki.
“Bado kuna makosa machache yanaonekana kwa mfano lile bao ambalo waliliruhusu kwenye mchezo uliopita, unawezaje kumlaumu kipa kirahisi wakati kuna watu walikuwa eneo lile lile alilokuwa mfungaji na wakashindwa kuisaidia timu, kocha yuko sahihi anatakiwa kuendelea kuiboresha timu yake.” Amesema Julio
Naye Boniface Pawasa amesema bado Simba SC ina kikosi kizuri lakini shida kubwa ambayo anaiona ni kwamba timu hijafanikiwa kushika vizuri falsafa za kocha Robertinho.
“Simba SC walizoea mpira wao wa kucheza pasi nyingi, kwa nyakati hizi wanapitia mabadiliko ya falsafa, huyu kocha anataka soka la kwenda mbele kwa kucheza na malengo, mashabiki wetu hawana ufahamu huo wao wanadhani timu yao bado itakuwa vilevile, naamini bado Simba SC ni timu bora na itakuja kuwashangaza watu,”amesema Pawasa ambaye ni beki wa zamani wa APR ya Rwanda.
“Kitu kingine nadhani wachezaji wenyewe wa Simba SC wanatakiwa kujitathimini, wanatakiwa kujiuliza watawezaje kuisaidia timu, sidhani kama wanastahili kukumbushwa jinsi ya kucheza kwa nidhamu sisi wakati tunacheza tulikuwa tunaulizwa mtaisaidiaje timu baada ya kutusajili? Hili Swali linatakiwa pia wajiulize wachezaji wa Simba SC.”