Kocha Mkuu wa KMC FC Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ amezichimba mkwara Simba SC na Young Africans kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa kusema hazitaambulia kitu.
Julio ametoa tambo hizo baada ya kufanikiwa kuibakisha KMC FC Ligi Kuu kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya City FC jana Ijumaa (Juni 16) katika mchezo wa Paly Off Mkondo wa Pili uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya mwanzoni mwa juma hili, KMC FC ilikubali kufungwa 2-1, hivyo imesalia Ligi Kuu kwa ushindi wa jumla wa 3-2.
Julio amesema kusalia kwa timu yake katika Michuano ya Ligi Kuu msimu wa 2023/24, ni hatua nzuri kwake, Wachezaji na Uongozi wa Klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni.
Amesema baada ya kuichukua timu hiyo siku chache kabla ya kukamilika kwa msimu wa 2022/23, amejitahidi kufanya alichokikusudia licha ya wachezaji waliopo hakuwasajili yeye, hivyo anaingia katika soko la usajili na atasajili wachezaji wenye viwango vya kuzizuia Simba SC na Young Africans katika vita ya Ubingwa Ligi Kuu na ASFC.
Amesema tangu akiwa Mwadui FC alikataa katakata kufungwa na Simba SC na Young Africans na alifanikiwa, hivyo kurejea kwake akiwa na KMC FC kunamfanya kuendelea na dhamira hiyo, lakini kwa msimu ujao amejipanga kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
“Huwa napata uchungu sana ninapoona timu za Tanzania kila siku zikienda kucheza nao basi lazima zifungwe na hizi Simba SC na Young Africans. Nilipokuwa Mwadui FC nilikataa kabisa kufungwa na timu hizi Simba na Young Africans ni timu kongwe na sio timu kubwa, wapeni salamu Julio atakuwepo Msimu ujao Ligi Kuu. Malengo yangu ni kubeba Ubingwa na KMC” amesema Julio