Mlinda mlango shujaa wa Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja Juma, ameendelea kupokea sifa na pongezi kutoka kwa wadau wa soka nchini kote, kufuatia mazuri aliyoyaonyesha kwenye mchezo wa jana dhidi ya Burundi.
Kaseja alipangua mkwaju mmoja wa penati, huku mikwaju mingine miwili ya Burundi ikienda nje ya lango, na kuifanya Tanzania kufuzu katika hatua ya makundi ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2022, zitakazounguruma nchini Qatar.
Mmoja wa wadau wa soka nchini ambaye amedhihirisha wazi furaha yake kwa mlinda mlango huyo mkongwe nchini, ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kumkabidhi Kaseja kiasi cha shilingi milioni 10 kama pongezi.
Makonda aliahidi kufanya hivyo mara baada ya mchezo wa jana dhidi ya Burundi, na leo mchana alimuita Kaseja ofisini kwake na kumkabidhi kitita hicho.
Baada ya Kaseja kupangua mkwaju wa penati, Makonda aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa, kipa huyo kwake ni mchezaji bora.
Mbali na kumtangaza hivyo, pia Makonda aliandika hapohapo kuwa kwa kiwango hicho kesho (leo) atamkabidhi kiasi cha Shilingi 10 milioni kama zawadi kwa kazi aliyoifanya.
Kaseja alifika ofisini kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akiambatana na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, kaimu kocha mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije na baadhi ya wachezaji wa Stars, Adi Yusuf, Himid Mao na Boniface Maganga na fedha hizo.
Hii ni mara ya pili kwa Makonda kutoa kiasi hicho cha fedha, aliwahi kufanya hivyo kwa kipa wa klabu ya Simba, Aish Manula.