Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amepingana na Baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo waliokata tamaa na Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Simba SC inapitia wakati mgumu wa kuangusha alama inapocheza ugenini, ikifanya hivyo jana Jumatano (Novemba 23katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City FC.
Akizungumza kabla ya kurejea jijini Dar es salaam akitokea jijini Mbeya, Mgunda alisema kikosi chake bado kina nafasi kubwa ya kulisaka taji la Tanzania Bara msimu huu, na atakuwa mtu wa mwisho kukubali kama wameshindwa kutimiza ndoto hizo.
Kocha Mgunda alisema ni dhahiri Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa na ushindani mkubwa kutokana na Timu Shiriki kuwa na Uwezo mkubwa wa kupambana, hivyo hana mashaka na hilo na badala yake anaendelea kuipambania timu ili ipate matokeo mazuri.
“Kutoa sare sio ‘Dhambi’ halafu tumecheza na Mbeya City ambayo nilitangulia kusema wana timu nzuri, kwa hiyo ifahamike kuwa mchezo ulikua mgumu na wenye ushindani na matokeo yamedhihirisha hilo.”
“Ushindani umeongezeka na bado tupo kwenye ushindani, niwambie kwamba tutapambana hadi mwisho na ‘HAIWI MWISHO HADI IFIKE MWISHO’.” alisema Mgunda
Matokeo ya 1-1 dhidi ya Mbeya City yanaifanya Simba SC kufikisha alama 28 zinazoiweka katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Azam FC yenye alama 29 sawa na Young Africans iliyo na michezo miwili mkononi.