Sekta binafsi nchini zimetakiwa kuwekeza katika sekta ya maji ili kuongeza wigo wa upatikanaji maji kwa wananchi hasa walioko vijijini.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa, idadi ya watanzania imeongezeka ukilinganisha na rasilimali maji zilizopo na hivyo inahitajika jitihada kubwa katika uwekezaji wa sekta hiyo ambapo ili ufanikiwe inatakiwa uwepo wa fedha za kutosha.
Amesema kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti katika sekta ya maji ili kutimiza lengo lake la kuwafikishia maji wananchi wote hasa wa maeneo ya vijijini.
Aidha, ameongeza kuwa serikali imepanga ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 ya watanzania wawe wamefikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Hata hivyo, kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo amesema ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya maji ni mdogo, ambapo pia alitoa wito kwa sekta hizo kuwekeza katika sekta ya maji hasa kwenye ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji.