Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wafanyakazi wa jumuiya hiyo wameacha kazi kutokana na kukabiliwa na ukata wa fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Steven Mlote amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote, hakuna mfanyakazi aliyeacha kazi na wale ambao hawapo wako likizo.

Amesema kuwa Jumuiya hiyo haina tatizo la ukata wa fedha kama taarifa zinavyoenezwa, kwani shughuli za jumuiya hiyo zinaendelea kama kawaida na wafanyakazi wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.

”Taarifa zilizosemwa kwamba wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekimbia ofisi sio za kweli, ukweli ni kwamba wako kazini, wanafanyakazi kwa weledi na Jumuiya iko salama na inaendelea kuimarika,”amesema Mlote

Aidha, kwa muda wa wiki moja sasa kumekuwepo na taarifa zinazosambaa kwamba wafanyakazi wa jumuiya hiyo wameikimbia ofisi kutokana na ukata wa fedha, ambao umesababisha wafanyakazi hao kutolipwa mishahara.

Hata hivyo, Mlote ameongeza kuwa changamoto zilizopo katika ofisi hiyo ni za kawaida, hivyo nchi wanachama wa jumuya hiyo zinaendelea kuchangia michango yake kama kawaida.

Jumuiya hiyo inaundwa na nchi wanachama, ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi.

 

Kampuni za simu zinazolalamikiwa kuibia wateja kuchunguzwa
Lissu atakiwa kufika Mahakama Kuu kesho, kutetea ubunge wake