Meneja wa mabingwa wa soka barani Ulaya (Liverpool) Jurgen Klopp amesema kikosi chake hakina budi kupambana kiamilifu katika michezo ya hatua ya makundi, ili kuondokana na aibu ya kutolewa mapema kwenye michuano ya bara hilo msimu huu.
Klopp ametoa kauli hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, kuelekea mpambano wa mzunguuko wa tatu wa ligi ya mabinbwa barani Ulaya hatua ya makundi dhidi ya KRC Genk, utakaochezwa leo usiku, nchini Ubelgiji.
Liverpool kwa sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E, kwa kuwa na alama tatu, baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya Red Bull Salzburg na SSC Napoli wanaoongoza msimamo wa kundi hilo.
“Mwaka 2018 tulipata wakati mgumu kwa kupoteza michezo ya ugenini, na ilituweka kwenye mazingira magumu, msimu huu tayari tumeshapoteza alama tatu dhidi ya SSC Napoli tulipocheza ugenini, kesho (Leo) tutakua ugenini hapa Ubelgiji, hivyo tunapaswa kuchukua tahadhari mapema ili tushinde mchezo huo,” alisema Klopp.
“Hatutaki kurudia makosa tulioyafanya mwaka 2018, ninaamini kwa msimu huu tunaweza kusitisha hiyo kasumba isijirudie tena.”
“Tunajua mara nyingi mchezo wa soka hukumu yake huegemea kwenye historia ya matukio, tutakua makini sana ili tukwepeshe hilo linalosemwa dhidi yetu.”
Katika mchezo wa leo dhidi ya KRC Genk, mshambuliaji Mohamed Salah anatarajiwa kurejea kikosini, baada ya kupona majeraha ya kifundo cha mguu, alioyapata majuma mawili yaliyopita.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, hakuwa sehemu ya kikosi kilichopambana dhidi ya Manchester United mwishoni mwa juma lililopita, na kila upande kuambulia alama moja, kufuatia sare ya bao moja kwa moja.
Beki wa kulia Trent Alexander-Arnold hatokua sehemu ya kikosi cha Liverpool akiungana na beki mwenzake Joel Matip ambao wanaendelea kujiuguza.
Beki Joe Gomez anatarajiwa kuziba nafasi ya Alexander-Arnold, huku Dejan Lovren akipewa nafasi kubwa ya kushirikiana na Virgil van Dijk kama mbadala wa Matip.
Kikosi cha Liverpool kinatarajiwa kuundwa na wachezaji waliosafiri hadi Ubelgiji kwa ajili ya mchezo huo: Alisson, Fabinho, Van Dijk, Wijnaldum, Lovren, Milner, Keita, Firmino, Mane, Salah, Gomez, Adrian, Henderson, Oxlade-Chamberlain, Lallana, Brewster, Robertson, Origi na Kelleher.