Imeelezwa kuwa huenda mfumo wa maamuzi wa VAR (Video Assistant Referee) ambao unatumika katika ligi kubwa za Ulaya ikiwemo England, Hispania na Italia, ukatumika kwenye mchezo wa Yanga na Simba Januari 4, mwakani.

Mipango inaendelea kuandaliwa kwa sasa kwa ajili ya VAR ambayo imekuwa ikiainisha makosa ambayo mwamuzi wa kati hayaoni, kutumika katika pambano hilo ambalo huteka hisia za mashabiki wengi Tanzania.

Taarifa za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia katibu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau ambaye amezungumza na moja ya chombo cha habari nchini amesema kwa sasa kuna mazungumzo ambayo yanaendelea kwa ajili ya VAR kutumika katika mechi hiyo ambayo itapigwa Uwanja wa Taifa ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 60,000.

“Bado hatujakubaliana ila kuna mazungumzo yanaendelea na Simba na Yanga kwa ajili ya VAR kutumika kwenye mechi yao.

“Muelekeo hadi sasa ni mzuri na hiyo itakuwa katika mechi zote za timu hizo zitakapokutana ikiwa ni kujaribu juu ya mfumo huo hapa nchini.

“Kuna uwezekano wa klabu hizo kukubali juu ya mfumo huo kwa ajili ya kuondoa utata wowote utakaojitokeza kwenye mechi hiyo.

“Ingawa haijathibitishwa kwa asilimia 100 lakini tunafikiria VAR itakuwepo katika mchezo huo na itatumika kwa majaribio japokuwa hatujajua huko mbele itakuwaje ila tutaanza kuitumia kwa majaribio katika mechi hiyo,” alisema Kidau.

Timu hizo mbili kwa mara ya kwanza zitakutana Januari 4, kwenye mechi ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wote kutokana na vikosi hivyo kila kimoja kufanya marekebisho makubwa.

Thiago Motta akabidhiwa jukumu zito Genoa FC
Wataalamu wa maendeleo ya jamii watakiwa kutoa takwimu sahihi