Aliyewahi kuwa Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Juuko Murshid ametangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ akiwa na umri wa miaka 27.
Juuko ametangaza kuachana na ‘The Cranes’ kupitia barua yake aliyoiwasilisha kwenye Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), na sasa ataendelea na jukumu moja tu, la kuitumikia klabu yake Express FC ya Uganda,
Katika Barua hiyo Juuko ameandika: “Nimeitumikia nchi vya kutosha na ni wakati wa mimi kupumzika”
“Haukuwa uamuzi rahisi lakini pamoja na familia yangu na uongozi wangu, tumefikiri na kuona ni uwamuzi sahihi. Ninawashukuru FUFA, wachezaji wenzangu na wadau wote wakati nilipokuwa na Uganda Cranes. Ninawatakia Uganda Cranes mafanikio mema, sasa akili yangu naielekeza katika klabu yangu ya Express FC”
Juuko amecheza michezo 39 akiwa na The Cranes na kufunga bao moja.
Alianza maisha yake ya soka katika Academy ya Entebbe, huku akizitumikia klabu za Vipers, Red Cross (mkopo), Sports Club Victoria University (SCVU), Simba (Tanzania) na Wydad Casablanca ya nchini Morocco.
Amecheza pia katika fainali mbili mfululizo za AFCON akiwa na The Cranes nchini Gabon (2017) na Misri (2019).
Pia alichezea timu za vijana za Uganda U-20 na U-23 kabla ya kuhitimu kucheza timu ya wakubwa (The Cranes) ambako alicheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Syechelles Julai 11-2014.
Utakumbuka hivi karibuni, FIFA ilimuadhibu kwa kumtoza faini Beki huyo, kufuatia kumpiga kiwiko mchezaji wa Timu ya Taifa ya Mali, Ibrahima Kone wakati wa mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, mchezo uliopigwa Uwanja wa St Mary’s, Kitende.