Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Juventus, Francesco Calvo amesema kuwa Meneja wa Kikosi cha klabu hiyo Massimiliano Allegri ataendelea na kazi yake licha ya tetesi kueleza huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa za awali zilieleza kuwa Uongozi wa Juventus FC ulikuwa una mpango wa kumtimua Massimiliano Allegri na nafasi yake kuzibwa na Meneja wa zamani wa Mabingwa wa Barani Ulaya Real Madrid Zinedine Zidane.
Allegri amekuwa akipambana kuona anairejesha Juventus kwenye ramani ya soka baada ya kuonekana kusuasua miaka ya hivi karibuni na kuziacha klabu za Inter Milan, AC Milan pamoja na SSC Lazio kutamba katika michuano ya ndani ya Italia.
Afisa huyo amesema Allegri bado ni Meneja wa kikosi chao na wataendelea kufanya naye kazi kwani huko nyuma alifanya makubwa akiwa Klabuni hapo.
Calvo amesema: “Massimiliano Allegri ataendelea kufanya kazi hapa kwa muda mrefu akiwa kocha wa timu hii.”
“Hakuna asiyejua kama Allegri alisaini dili la miaka minne, hivyo hata nusu bado hajafikisha, kwa sasa anaendelea kupambana.”
“Mataji 11 ametwaa akiwa hapa, kumbuka ametupeleka fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, hivyo sio kitu kidogo.”