Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia Kidato cha Nne hadi Shahada ya Uzamili ambao wamemaliza Mkataba wa Mafunzo ya Kujitolea JKT na kurudishwa majumbani.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Machi 9, 2023 Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano na Msemaji Mkuu Jeshi la wananchi – JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema muombaji anatakiwa awe Raia wa Tanzania wa kuzaliwa, mwenye Kitambulisho cha Taifa, na umri wa miaka 18 – 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne – sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.
Amesema, “Awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na vyeti vya Taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo pia awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa kujitolea miaka miwill (2) na kutunukiwa cheti”, amesema Ilonda
Amesema maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiwa na viambatisho ikiwemo nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA.
“Natambua kuwa baada ya tangazo hili kuna mwanya wa matapeli utaibuka na watapenda kutumia fursa hii, nawaomba Watanzania kukataa kurubuniwa kwani hakuna njia ya mkato katika kupata nafasi hizi,” amesema Ilonda.