Kesi inayowakabili viongozi wa Klabu ya Simba, Rais Evans Elieza Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu.
Upande wa mashtaka leo uliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwamba jalada la kesi ya utakatishaji fedha na kugushi nyaraka limeshatoka katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na kurejeshwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mwendesha Mashitaka, Wakili Leonard Swai alisema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kwamba shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Swai alidai kuwa jalada hilo lilirudishwa TAKUKURU, juzi kutoka kwa DPP ambaye ametoa maelezo ya kukamilishwa zaidi kwa upepelezi.
Maelezo hayo ya upande wa mashitaka yalitolewa baada ya wakili wa utetezi, Philemon Mitakyamirwa kuhoji kuhusu jalada la kesi hiyo ambalo ilielezwa kuwa lipo kwa DPP, hivyo alitaka kujua hatua zilizofikiwa.
Ikumbukwe, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wapo rumande gereza la Keko tangu Juni 29.
Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za kugushi kwa uongozi Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
Kwa sasa nafasi zao zinakaimiwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ kama kamu Urais na Iddi Kajuna kama kaimu Makamu wa Rais.