Makamu wa Rais wa klabu ya Simba Geoffrey Nyange Kaburu, amekanusha taarifa za kuondoka kwa wachezaji watatu wa klabu hiyo Ibrahim Ajib Migomba, Jonas Gerard Mkude na Abdi Hassan Banda katika kipindi hiki cha usajili.
Kaburu amekanusha taarifa hizo, kufuatia baadhi ya vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa za uwezekano wa kuondoka kwa wachezaji hao ambao inadaiwa huenda wakajiunga na klabu za Singida Utd, Young Africans pamoja na kusaka maisha mapya nje ya nchi (Afika Kusini).
Mshambuliaji Ibrahim Ajib amekua akihusishwa na taarifa za kutaka kusajiliwa na klabu ya Singida Utd, Jonas Mkude anadaiwa kuwaniwa na Young Africans na Abdi Banda anajipigia debe la kusajiliwa na moja ya klabu huko Afrika kusini.
Kaburu amesema tayari wachezaji hao watatu wameshaanza mazungumzo ya kusaini mikataba mpya ambayo itawawezesha kuendelea kuitumikia klabu ya Simba kwa kipindi kingine, na amesisitiza kuwa katika hatua nzuri ya kukamilisha mpango huo.
“Hakuna mchezaji hata mmoja atakaeondoka, wote wapo katika hatua nzuri ya kusaini mikataba mipya, tunataka kuona Simba inaendelea kuwa imara kwa kuwatumia watu hawa ambao msimu huu wameonyesha kuwa muhimili mkubwa katika klabu yetu.”
“Taarifa za kutaka kuondoka, sisi kama viongozi tunazisikia na kuziona katika vyombo vya habari, lakini ninakuhakikishia hakuna hata mmoja atakaeondoka katika kipindi hiki.” Kaburu aliiambia Times FM.
Hata hivyo kwa upande wa Abdi Banda ambaye kwa sasa yupo Misri na timu ya taifa, amesisitiza kuondoka klabuni hapo na kusema mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa Simba aliezungumza nae kuhusu mpango wa kusaini mkataba mpya.
Banda amesema lengo lake kwa sasa ni kwenda Afrika kusini kucheza soka, na akipata nafasi atakuwa tayari kucheza soka popote pale lakini sio ndani ya Tanzania.
Hata hivyo amekiri kuwa na ofa ya moja ya klabu za ligi kuu ya soka Tanzania bara, lakini hakua tayari kuitaja japo ametanabaisha kwamba, kwa sasa haifikirii ofa hiyo na badala yake anawaza kwenda nje ya nchi kucheza soka lake.
Kwa upande wa Jonas Mkude na Ibrahim Ajib wameendelea kukaa kimya na hawajazungumza kwa kina kuhusu mpango wa kutakiwa na klabu nyingine hapa nchini, japo kuna tetesi zinazoitaja klabu ya Young Africans na Singida Utd kuhusika na uhamisho wa wawili hao.