Baada ya kukamilika kwa fainali za mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 zilizofanyika nchini Gabon katika miji ya Libreville na Port Gentil, kamati ya soka la vijana visiwani Zanzibar imetoa tamko la kujifunza jambo kupitia michuano hiyo.

Katibu mkuu wa kamati ya soka la vijana visiwani humo Abdallah Sunday, amesema yapo mengi waliyojifunza kupitia fainali hizo, na wanaamini ushiriki wa Zanzibar kama nchi kwa ajili ya fainali za mwaka 2019 zitakazofanyika Tanzania bara utakua na kila sababu kufanya vizuri.

Sunday amesema anaamini Zanzibar ina vipaji vingi vya soka, jambo ambalo litasaidia katika mpango wa kuviwezesha visiwa hivyo vya bahari ya Hindi kupambana na kufuzu kucheza fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 za mwaka 2019.

“Hatuna budi kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutujaalia vijana wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka, jambo hili ni kama bahati kwetu, tuna kila sababu ya kutumia baadhi ya mambo tuliyojifunza katika michuano ya AFCON kwa vijana ambayo imemalizika siku chache kule Gabon, ili kufanikisha ndoto zetu.”

“Kubwa ambalo kamati yangu imejifunza ni kuwatengeneza wachezaji ili watambue uzalendo wao, na tukifanikiwa hivyo hakuna litakaloshindikana kabisa katika mpango wa kufuzu kucheza fainali zijazo.” Amesema Sunday.

Kuhusu mpango wa kuandaa kikosi Sunday amesema tayari wameshaagiza kila wilaya ya Zanzibar kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13, 15 na 20 ambao watapambana kwa kigezo cha umri wao, na kisha watachujwa na kufikia lengo la kuundwa kwa kikosi cha timu ya taifa ya visiwa hivyo.

Zanzibar itashiriki kama nchi katika michezo ya kuwani kufuzu fainali za vijana za Afrika za mwaka 2019, baada ya kupata sifa ya kutambuliwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF kama mwanachama kamili.

Endapo Zanzibar itafanikiwa kufuzu kucheza fainali zinazo za vijana chini ya umri wa miaka 17, Tanzania itakua na wawakilishi wawili kwenye fainali hizo, kwani Serengeti Boys itashiriki kama nchi mwenyeji.

Video Mpya: Rin Marii Afungua Pazia na Wimbo wa ‘Salaam’
Kaburu: Hang'oki Mtu Msimbazi