Kaimu Mwenyekiti wa klabu bingwa Tanzania Bara Simba SC, Mwina Seif Mohamed Kaduguda amesema, bado hawajapata taarifa rasmi kuhusu mchezaji wao wa zamani Shiza Kichuya kufungiwa na Shirikisho la Soka duniani (FIFA), pamoja na wao kutakiwa kulipa faini ya dola za kimarekani 130,000 sawa na shilingi milioni 300.
FIFA walitangaza adhabu hiyo mwanzoni mwa juma hili, baada ya kutoa hukumu ya kesi iliyowasilishwa kwao na klabu Pharco ya Misri, ambayo mshambuliaji huyo aliwahi kuitumikia akitokea Simba SC.
Shauri hilo lilikuwa linafanyiwa uchunguzi na Kamati maalumu ya DR Congo iliyo chini ya FIFA kabla ya kutoka kwa maamuzi ya faini hiyo ya Kichuya kufungiwa.
Kaduguda amesema: “Taarifa hizo bado ni mpya kwetu, Bodi ya Wakurugenzi hatujapokea taarifa rasmi kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wetu, Barbara Gonzalez, hivyo tunasubiri taarifa rasmi ifikishwe kisha tutakaa kuijadili.
“Ila tunawaomba mashabiki wa Simba wawe watulivu kwa sababu maamuzi kama haya yanafanyika lakini hayamaanishi kuwa yapo sahihi.
“Kuna wakati maamuzi yanaweza kufanyika na yasiwe sahihi na ndiyo maana ipo nafasi ya kuweza kukata rufaa na maamuzi yakabadilishwa baada ya kupitiwa upya, nisingependa kuongea mengi kwa sasa tusubiri Barbara atalitolea ufafanuzi,” amesema.
Kwa sasa Kichuya anacheza ndani ya Namungo ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Bara ikiwa chini Kocha Mkuu, Hemed Morroco.