Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ imehamisha michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ya Kagera Sugar kutoka Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera na kuipeleka Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
TPLB imechukua maamuzi hayo, kufuatia sababu za kiusalama baada ya kuthibitisha kuwa uzio wa kutenganisha Mashabiki na eneo la Kucheza (Pitch), haujakidhi vigezo vya Kikanuni.
Hata hivyo Taarifa ya TPLB imeeleza kuwa, mchezo Namba 36 kati ya Wenyeji Kagera Sugar dhidi ya Singida Big Stars unaochezwa leo Ijumaa (Oktoba 21), utachezwa Uwanja wa Kaitaba bila Mashabiki.
Baada ya mchezo huo Kagera Sugar itaanza safari ya kuelekea jijini Mwanza na kuanza kuutumia Uwanja wa CCM Kirumba kwa michezi yake ya nyumbani, hadi Kamati ya Leseni za Klabu itakapoukagua Uwanja wa Kaitaba na kujiridhisha mapungufu yaliyowasilishwa yamerekebishwa.
Katika hatua nyingine Bodi ya Ligi Kuu ‘TPLB’ imewaondoa hofu Mashabiki wa Soka waliokua wamekata Tiketi za kushuhudia mchezo wa leo Ijumaa kati ya Kagera Sugar dhidi ya Singida Big Stars, kwa kusisitiza itahakikisha wanarudishiwa haki yao.