Idara ya Habari na Mawasilino ya Kagera Sugar imewataka Mashabiki wa klabu hiyo kuwa tayari kwa usajili utakaotangazwa wakati wowote kuanzia sasa.
Kagera Sugar ni miongoni mwa Klabu za Ligi Kuu zilizotangaza kuachana na Wachezaji wengi katika kipindi hiki, huku ikiendelea kusajili kwa kuziba nafasi zilizoachwa wazi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino Klabuni hapo Hamis Mazanzala amesema, usajili wa Wachezaji wapya klabuni hapo umekamilika kwa asilimi 80, kulingana na mapendekezo ya Kocha Mkuu Franciss Baraza.
Mazanzala amewatoa hofu Mashabiki wa Kagera Sugar kwa kusema, waliosajiliwa klabuni hapo wana hadhi kubwa, na wataweza kuifikisha mbali klabu yao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
“Tunaendelea kufanya usajili kwa mapndekezo ya Kocha Baraza, tayari tumeshakamilisha usajili wa wachezaji wapya kwa asilimia 80, wakati wowote wataanza kutangazwa kupitia vyanzo vyetu vya habari, mashabiki wanapaswa kutulia.”
“Benchi la Ufundi limependekeza wachezaji wazuri ambao walifanya vizuri huko tulikowatoa, binafsi sina hofu kabisa, pia niwatoe hofu mashabiki wetu, tutakua na timu bora na imara msimu ujao.” amesema Mazanzala
Hata hivyo inaelezwa kuwa Kagera Sugar imemsajili Mshambuliaji wa Dodoma Jiji Anuwar Jabir, Mpapi Nassib na Judika Mafie wote wanatoka Biashara United Mara na Datius Peter kutoka Polisi Tanzania.
Wachezaji walioachwa Kagera Sugar katika kipindi hiki ni Peter Mwalianzi, Cosmas Lewis, Hassan Mwatelema, Nassoro Kapama, Mwaita Gereza, Erick Kyaruzi, Sadat Nanguo, Yusuph Mlipili, Nurdin Barola na Jordan John.