Serikali Mkoani Kagera, imepokea kiasi cha shilingi 2 Bilioni toka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa kituo tengefu ili kukabiliana na Magonjwa ya milipuko, ambayo yamekua yakitokea mkoani humo ukiwemo Marburg na magonjwa mengine.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila katika kikao na Watumishi wa idara ya Elimu na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Mkoani Kagera, cha kujadili namna ya uboreshaji wa miundombinu kwa shule za msingi baada ya serikali kutoa kiasi cha zaidi ya bilioni 10 kupitia mradi wa “boost”.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila.
Amesema, “Rais amekwisha hidhinisha na kutoa fedha bilioni 2 kwa ajili ya kuanza ujenzi, katika ujenzi huu kuna maeneo tunataka tuyatambue, moja ya maelekezo yangu kwenu tutahitaji eneo lisilopungua heka 10 linaloweza kutokuwa mbali na barabara kuu, na itakuwa senta isiyozidi bilioni 7 mpaka 10.”
Baadhi ya Wakurugenzi na Maafisa elimu kwenye kikao cha fedha za booster kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera.
Aidha, Chalamila ameongeza kuwa, “wakurugenzi wa bukoba vijijini,bukoba manispaa,missenyi na karagwe wanatakiwa kubainisha maeneo hayo ili kutokwamisha zoezi hilo,” huku Wakurugenzi wa Missenyi na Ngara wakisema agizo hilo litafanyiwa kazi, ili kurahisisha utekelezaji wa kutatua changamoto za magonjwa ya mlipuko.