Mshambuliaji wa klabu bingwa Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC, Meddie Kagere amesema amesikitishwa na taarifa zilizosambaa mtandaoni kuwa amempiga kocha wa timu hiyo, Sevn Vandenbroeck.
Jana taarifa za Kagere kudaiwa kumpiga kocha huyo kisa kikiwa ni kutopangwa kikosi cha kwanza cha Simba zilizagaa kwa kasi mitandaoni, na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari mapema hii leo.
Akizungumza na E.A Radio mapema hii leo, mshambuliaji huyo kutoka Rwanda alisema ameshangaa baada ya kuona mambo hayo yanasambaa wakati yeye hajafanya tukio hilo na yuko freshi kabisa na kocha.
“Kuna mambo huwa yanasemwa kuhusu mimi ambayo siyo ya kweli yenye lengo la kunichafua ndiyo maana sijawahi kuwajibu.”
“Lilianza la hirizi nikanyamaza na sasa limekuja la mimi kupigana na kocha kitu ambacho siyo kweli. Tangu tumefika Mbeya hatujafanya mazoezi na leo muda huu ndiyo tunafanya sasa nashangaa sijui mwalimu nimempiga wapi,” alisema Kegere.
Hata hivyo Uongozi wa Simba SC kupitia idara ya habari na mawasiliano umekanusha taarifa hizo kwa kusema hazina ukweli, zidi ya kutaka kuvuruga amani ndani ya kikosi chao ambacho kipo tayari kuanza kutetea taji la Tanzania Bara mwishoni mwa juma hili dhidi ya Ihefu FC.
Mkuu wa Idara hiyo Haji Manara amesema: ”Wanasema jana ugomvi uliotokea mazoezini, lakini Simba hawakuwa na mazoezi baada ya mchezo wa ngao ya jamii, hizo ni propaganda za kuvuruga utulivu uliopo ndani na nje ya Simba, wakitaka itokee kama upande wa pili yanayoendelea”
“Kama idara ya Habari na Mawasiliano hatutokubali kuona watu wanaandika uzushi kuhusu Klabu yetu na tutachukua hatua kali dhidi ya watakaohusika”