Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda na klabu ya Simba SC Meddie Kagere amesema yupo tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa pili hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly, utakaochezwa kesho Jumanne (Februari 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es salaam.
Kagere amesema endapo kocha Gomez atampa nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi, atahakikisha anafanya jitihada kwa kusaidiana na wenzake, ili kutimiza lengo la ushindi katika uwanja wa nyumbani.
Amesema anatambua mchezo utakua mgumu kulingana na wapinzani wao kuwa na uzoefu wa kutosha wa kucheza nyumbani na ugenini, lakini maandalizi wanayoendelea kuyafanya, yanampa matumaini ya kuamini Simba SC itafanya vyema.
“Kama nitapata nafasi ya kucheza katika mchezo wa kesho Jumanne na tukatengeneza nafasi hata kama zikiwa chache kama ilivyokuwa mara ya mwisho naweza nikawapa furaha mashabiki wetu kwa kufunga bao tena. Tunataka kushinda tena tukiwa nyumbani,” amesema Kagere.
“Unajua tunakwenda kucheza na timu bora hapa Afrika iliyokamilika katika maeneo yote kwa maana hiyo tutakwenda kukutana na ushindani wa kutosha kutoka kwao ambao utachangia kutengeneza nafasi chache za kufunga na kama nitakutana na moja kati ya hiyo nitahakikisha naitumia,” amesema.
“Tumeweza kushinda ugenini ikiwa ni mwanzo mzuri kwetu kwani miongoni mwa malengo ambayo tulikuwa nayo huko walau tusiondoke bila ya pointi moja lakini tumefanikiwa kupata tatu. Tukifanikiwa kucheza vizuri na kuwafunga Al Ahly ni wazi tutamaliza vyema kwenye kundi letu.”
Kagere amesema kumaliza kileleni mwa kundi kuna faida mbili ya kwanza katika hatua ya robo fainali unapangiwa na timu ambazo hazina ubora, lakini hata mchezo wa kwanza katika hatua hiyo utaanzia ugenini na kumalizia nyumbani.
Kagere ndiye aliyefunga bao pekee lililoizamisha Al Ahly katika mchezo wa michuano hiyo msimu wa 2018-2019 uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 12, 2019.