Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhan Kailima ametoa wito kwa watumishi wa umma na Watanzania kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi wenye sifa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kailima amesema hayo Mjini Dodoma baada ya kujiandikisha katika daftari hilo kwenye kituo kilichopo Mtaa wa Chimuli, Kata ya Makole.
Amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla, lakini uzoefu unaonyesha kuwa kuna mwamko mdogo kwa kundi la watumishi wa umma kujiandikisha, kushiriki uchaguzi huo ili waweze kuchagua viongozi wenye sifa.
“Kampeni zitafanyika kwa wiki moja kuanzia Novemba 17-23, mwaka huu, uchaguzi utafanyika Novemba 24, mwaka huu…ni muhimu jamii kutambua kuwa, mshindi katika uchaguzi huu atapatikana kwa idadi ya wapiga kura sio asilimia,” amesema.
Kailima amesema ni muhimu Watanzania wakashiriki uchaguzi huo uli watumie fursa hiyo kuchagua kiongozi anayestahili, wasiposhiriki atachaguliwa Mwenyekiti wa Serikali ama mjumbe ambaye jamii kubwa haitapenda achaguliwe.
“Nawaomba wananchi wahudhurie kampeni, waulize maswali kwa wagombea, watumie fursa hiyo kuchagua viongozi ambao ni waadilifu na waaminifu.”
Aidha, Kailima amewaonya wananchi kutojihusisha kupokea rushwa kutoka kwa yeyote. “Rushwa ni adui wa maendeleo, wananchi mjiepushe kupokea rushwa, Wizara yangu kupitia taasisi zake za ulinzi na usalama ziko imara, tutaimarisha ulinzi wakati wa kampeni, upigaji kura na utangazaji matokeo,” alifafanua.
Pia amewapongeza waandikishaji, wasimamizi wa zoezi hilo kwa kufika mapema kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura.
Amesema vituo hivyo viko sehemu za barabarani, mitaani ambapo uandikishaji huo hauna vikwazo kwani hauhitaji kitambulisho cha uraia, cheti cha kuzaliwa.