Uongozi wa klabu ya AC Milan ya Italia, umemtangaza Stefano Pioli kuwa meneja, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Marco Giampaolo alietimuliwa klabuni hapo siku ya jumanne, baada ya kuhudumu kwa muda wa miezi mitatu na nusu.

Pioli, raia wa italia mwenye umri wa miaka 53, anakuwa meneja wa tisa, tangu klabu ya AC Milan ilipotwaa ubingwa wa “Serie A” kwa mara ya mwisho mwaka 2011.

Meneja huyo ambaye amewahi kuvinoa vikosi vya klabu za klabu za Inter Milan, Fiorentina na Lazio amesemaini mkataba wa miaka miwili, kwa lengo la kuirejesha AC Milan kwenye ushindani wa kweli.

Meneja huyo mpya atawajibika kurekebisha makosa yote ndani ya kikosi cha AC Milan, ili kufanikisha mipango itakayoiondoa klabu hiyo kwenye nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ya Serie A, huku kukiwa na tofauti ya alama tatu dhidi ya timu zilizo kwenye ukanda wa kushuka daraja.

Mwishoni mwa juma lililopita AC Milan iliifunga Genoa mabao mawili kwa moja, huku mlinda mlango Pepe Reina akiokoa mkwaju wa penati dakika za lala salama, na kuifanya klabu hiyo kupata ushindi watatu msimu huu, kwenye michezo saba waliyocheza.

Tayari AC Milan wamepoteza michezo mitatu dhidi ya wapinzani wao wa jadi Inter Milan, Torino na Fiorentina.

Menejan aliyetimuliwa klabuni hapo Giampaolo mwenye umri wa miaka 52, alitangazwa kuchukua nafasi ya Gennaro Gattuso mwezi Juni mwaka huu, baada ya mchezaji huyo wa zamani kujiuzulu, kufuatia kushindwa kufika malengo ya kuipeleka timu yake katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Giampaolo aliisaidia Sampdoria kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ya Italia msimu uliopita, na aliaminiwa huenda angekua dawa ya tatizo la timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwa kipindi kirefu.

AC Milan ambayo tayari imeshatwaa ubingwa wa Ulaya mara saba, haijashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani humo tangu msimu wa 2013-14.

Msimu huu klabu hiyo ilipaswa kushiriki michuano ya Europa League, lakini imekwamishwa na adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja na shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA), kufuatia kosa la kuvunja sheria ya matumizi ya fedha (Financial Fair Play).

Kailima atoa wito kwa watumishi wauma, wananchi kujiandikisha
NEC: Kadi ya mpiga kura haitatumika kwenye uchaguzi serikali za mitaa