Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano litakalo wajumuisha walimu wa shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi ambalo litazungumzia changamoto ya ukatili kwa watoto.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa shule za Rightway, Mercy Mchechu wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na shirika liliso la kiserikali la Mine Foundation, kongamano hili linatarajiwa kufanyika Desemba 15, 2022 jijini Dar es Salaam.
Amesema, lengo la kongamano hilo ni kushirikishana mbinu mbalimbali za kuwalinda watoto dhidi ya ukatili hasa wakiwa maeneo ya shule.
” Walimu wananafasi kubwa ya kukomesha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto mashuleni ikiwa watashirikishwa kwa kupewa taarifa sahihi na mbinu za kutumia ili waweze kuwajengea watoto uwezowa kutambua ukatili na kuutolea taarifa pindi utakapo jitokeza na hili ndiyo lengo la kongamano hili” amesema Mchechu.
Naye Meneja wa Mine Foundation, Joab Ndazi amesema kuwa mada na mijadala katika kongamano hilo itaendeshwa na wataalamu kutoka Dawati la Jinsia Polisi, Ustawi wa jamii, Shirika la HakiElimu na wadau wengine.
Kwa mujibu wa Takwimu za shirika la HakiElimu mwaka 2020, zilibaini uwepo wa matukio ya unyanyasaji wa watoto katika mifumo tofauti, takribani asilimia 87.9 ya watoto wamewahi kukumbana na ukatili wa kikatili husasa ni kupitia adhabu ya viboko, asilimia 17.0 ya watoto walio shule za umma na asilimian 14.3 walio shule binafsi wamewahi kunyanyaswa kingono angalau mara moja wakati ailimia 34.3 ya watoto wa shule kwa ujumla wamenyanyaswa kisaikolojia hasa na wazazi au walezi.