Uongozi wa Klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini umedhamiria kumpa ajira Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi.
Uongozi wa Klabu hiyo ambayo imeshindwa kutamba katika soka la Afrika Kusini kwa miaka kadhaa sasa, unapanga kumuajiri Kocha huyo kutoka nchini Tunisia, huku ukijipanga kuachana na Kocha wao wa sasa Arthur Zwane.
Taarifa zilizoripotiwa kutoka Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini ‘SABC’ zinaeleza kuwa Uongozi wa Kaizer Chiefs upo katika mazungumzo na wawakilishi wa Kocha huyo, ambaye jana Jumatatu (Juni 12) aliizawadia Young Africans taji la pili la Kombe la Shirikisho Tanzaia Bara ‘ASFC’ tangu alipotua klabuni hapo miaka miwili iliyopita.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanayoendelea sasa ni kuhusu makubaliano binafsi ya Kocha huyo, ambaye atakuwa huru kunzia mwezi Julai, baada ya mkataba wake na Young Africans Africans kufikia kikomo.
Inaelezwa kuwa Amakhosi wamefanya haraka kujaribu kupata huduma ya Kocha huyo, baada ya kuthibitishwa kuwa alikuwa na nia ya kuondoka Young Africans baada ya kipindi kingine cha mafanikio, ambacho kimehitimishwa kwa mataji matatu mfululizo.
Nabi pia ameiwezesha Young Africans kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kufungwa na USM Alger katika mechi mbili za awali mapema mwezi huu.
Nabi, mwenye umri wa miaka 57 anayeitwa ‘Profesa’ amewahi kufanya kazi Sudan, Misri na Libya, lakini mafanikio aliyoyapata Young Africans ndiyo yamempandisha hadhi Barani Afrika.