Mlinda Lango chaguo la Pili wa Simba SC Beno Kakolanya ametoa msukumo kwa Viongozi wa Klabu hiyo kuanza mchakato wa kumsaka Mlinda Lango mbadala, kufuatia taarifa kueleza yu njiani kuondoka Msimbazi.

Taarifa zinaeleza kuwa hofu imetanda klabuni hapo ya kumkosa Mlinda Lango huyo namba mbili kufuatia Kakolanya kutajwa kuwa mbioni kujiunga na Singida Big Stars kwa mkataba wa miaka miwili, huku mkataba wake na Simba SC ukitarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu 2022/23.

Hofu ya mabosi hao imekuwa baada ya Mlinda Lango huyo kutokuwa kwenye msafara wa Simba SC uliokuwepo kwenye mchezo juzi Jumatatu dhidi ya Ihefu FC ambao timu hiyo ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0.

Taarifa hizo zimeongeza kuwa mabosi wa timu hiyo ambao kwa sasa ameanza kupambana kuhakikisha anabakia kwenye timu huku yeye akitoa masharti yake.

“Ni kweli Kakolanya amezua hofu kwa mabosi wa juu kwa sababu wameshajua kama amesaini mkataba na Singida na tayari ameshawekewa pesa ambayo wamekubaliana na kinachosubiliwa ni ligi kumalizika ili aweze kujiunga nao.”

“Lakini wamekuwa na mazungumzo na kipa mwingine wa kigeni kutoka nje kama itashindikana kumrudisha Kakolanya kwa kurudisha pesa alizochukua basi watamchukua huyo kipa ingawa Kakolanya amewapa masharti yake ikiwa wanataka abakie kwenye timu,” amesema mtoa taarifa.

Kwa upande wa Meneja wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kwa sasa suala hilo bado halijafika kwenye meza yake hivyo hawezi kuzungumzia chochote.

“Binafsi bado halijafika kwenye mezani yangu kwa sababu pengine linashughulikiwa na uongozi wa juu ila kwa sasa sijui chochote juu ya jambo hilo,” amesema Ahmed Ally

Maguire amesoma alama za nyakati Man UTD
Polisi yamsaka aliyeiba Silaha iliyosalimishwa na risasi 10