Mgombea ubunge wa jimbo la Monduli kwa tiketi ya CCM, Julius Malanga amemrudia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akijibu tuhuma alizozitoa dhidi yake kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho kikuu cha upinzani.
Kalanga ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema na baadaye kujiuzulu na kuhamia CCM amesema kuwa Lowassa amemchafua kwa kutumia utajiri alionao.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mto wa Mbu, Kalanga alisema kuwa amezungumza na wazee wa kimila wa Monduli, na kuwaeleza namna ambavyo Lowassa anatumia utajiri wake kumtuhumu kwa uongo kuwa alijiuzulu baada ya kushindwa kulipa deni la Sh.600 milioni.
“Nimezungumza na wazee wa kimila kuhusu jinsi ambavyo Lowassa ametumia utajiri wake kunichafua. Lowassa anasambaza habari za uongo kuwa nilijiuzulu kwa sababu nilishindwa kulipa deni la Sh600 milioni,” alisema Kalanga mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika uzinduzi wa kampeni za Chadema, Lowassa alidai kuwa alipata habari mapema kuwa Kalanga amepanga kujiuzulu nafasi yake na kwamba alimpigia simu na kumuuliza juu hilo, “aliniambia hapana mzee.”
Alisema baadaye aliambia amejiuzulu tayari na kwamba sababu ni kutaka alipiwe deni la Sh600 milioni.
Mwanasiasa huyo mkongwe alienda mbali na kudai kuwa Kalanga anapenda starehe na kwamba fedha hizo alichukua mkopo na kununua ng’ombe ambazo zilikufa na fedha nyingine alifanyia starehe jijini Arusha.
Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka takribani 20 andiye aliyemsimika Kalanga kurithi nafasi yake katika kampeni za mwaka 2015 baada ya wawili hao kuhamia Chadema wakitokea CCM.
Wananchi wa Monduli wanatarajia kumchagua mbunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16.