Serikali ya Tanzania imezishukuru nchi za Ufaransa na Norway kwa mchango wao mkubwa walioutoa na wanaoendelea kuutoa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa shukrani hizo wakati wa kikao baina yake na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier pamoja na Bjorn Midthun, ambaye ni Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Norway nchini.
“Mmefanya kazi nzuri sana katika kutuwezesha kutekeleza miradi ya umeme vijijini, ushirikiano wenu umetuwezesha kufikia hatua hii tuliyopo leo kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru sana,” amesema Kalemani.
Dkt. Kalemani amesema hadi sasa zaidi ya vijiji 9,512 ambavyo ni zaidi ya asilimia 85 ya vijiji vyote 12,268 vilivyopo nchini, vimeshafikiwa na umeme.
Amesema umeme ni injini ya uchumi huku akipambanua kuwa pasipo umeme wa uhakika, haiwezekani kwa nchi yoyote kuwa na maendeleo ya kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Balozi Clavier pamoja na Midthun, wamemhakikishia waziri Kalemani kuwa serikali za nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha miradi mbalimbali ya umeme.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Styden Rwebangira, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)