Kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC Kally Ongala ametoa sababu ya kikosi chake kushindwa kutinga Fainali Kombe la Mapinduzi 2023.
Azam FC ilipoteza mchezo huo wa kwanza wa Nusu Fainali kwa kipigo cha 4-1 kutoka kwa Singida Big Stars inayotinga kwa mara ya kwanza Fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Kocha Kally amesema Kikosi chake kilicheza chini ya kiwango cha kupelekea Singida Big Stars kupata mabao yote kwa urahisi, hivyo hana budi kuipongeza timu hiyo kutoka mkoani Singida.
Amesema kutokana na mapungufu alioyaona kwenye mchezo huo hana budi kuyafanyia kazi kabla ya kuendelea na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utarejea tena juma lijalo.
“Hatukucheza vizuri kwa kweli, tuliwapa nafasi wapinzani wetu na walituadhibu kwa mabao ambayo ninasema yamepatikana kirahisi sana, kwa hiyo ninapenda kuipongeza Singida Big Stars kwa ushindi walioupata dhidi yetu.”
“Nimeona tulipojikwaa kwa kushirikiana na wenzangu katika Benchi la Ufundi tutahakikisha tunayafanyia kazi mapungufu yetu ili kuwa sawa kabla ya kuendelea na Ligi Kuu.” amesema Kally
Wakati huo huo kikosi cha Azam FC leo Jumatatu (Januari 09) kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’ na baadae kuanza safari ya kurejea jijini Dar es salaam.