Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ amesema anafurahia kufanya kazi na Kocha Mzawa Juma Ramadhan Mgunda.

‘Robertinho’ Rasmi ameanza kazi ya kukinoa kikosi cha Simba SC jana Jumapili (Januari 08) kambini Falme za Kiarabu (Dubai).

Akizungumza na Kuptia Simba TV Kocha huyo amesema Kocha Mgunda amekua mwenyeji wake mzuri na ameona kuna mambo mengi mazuri kutoka kwake, ambayo yatamsaidia katika Mchakamchaka wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.

“Kila muda ninapenda kuwa naye kwa sababu ana uzoefu wa kutosha katika soka la Afrika, ni Rafiki na kaka yangu pia, ninaamini tutafanya kazi nzuri.” amesema ‘Robertinho’

Wakati huo huo Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62 amewahimiza Wachezaji wa simba SC kuwa kitu kimoja ili kufanikisha lengo la kufanya vizuri katika Michuano ya Ligi Kuu na ile ya Kimataifa.

Amesema tayari ameshakaa chini na wachezaji wote na kuzungumza nao kuhusu ushirikiano, huku akiamini uwezo na ujuzi uliopo kikosini kwake utafanikisha mipango aliyojiwekea, sambamba na Benchi lake la Ufundi.

“Kazi nzuri kwa kocha yoyote ni kuonesha heshima kwa Wachezaji na Wachezaji kumuheshimu kama Kocha, kukiwa na ushirikiano wa namna hiyo kila kitu kitakua kizuri ndani na nje ya Uwanja.”

“Nimewaambia kila kitu kuhusu Ushirikiano baina ya wao kwa wao, kama watashindwa kufanya hivyo basi hatutaweza kufanya lolote hata kama tutakuwa na Wachezaji wazuri kiasi gani.” amesema ‘Robertinho’

Simba SC imeweka Kambi ya Juma moja Falme za Kiarabu, huku ikitarajia kucheza mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Januari 17, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kally Ongala: Tumefungwa kirahisi sana
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Januari 9, 2023