Mshambuliaji wa zamani wa Klabu ya Juventus ya Italia Gianluca Vialli amefarikia Dunia akiwa na umri wa miaka 58.

Gwiji huyo wa Soka nchini Italia amefikwa na umauti ikiwa ni juma moja baada ya Gwiji wa Soka nchini Brazil na Duniani kwa ujumla Edson Arantes Do Nascimento ‘Pele’ kufarikia Dunia.

Taarifa zinaeleza kuwa Vialli ambaye pia aliwahi kuzitumikia Klabu za Cremonese (1980–1984), Sampdoria (1984–1992) na Chelsea (1996–1999), kwa kipindi kirefu alikuwa anasumbuliwa na Ugonjwa wa Saratani.

Tangu 2018 alikuwa akipigana na saratani ya Kongosho ambayo katika siku za hivi karibuni ilikuwa mbaya zaidi, hadi kupelekea kulazwa Hospitalini.

Rais wa Shirikisho la Soka nchini Italia ‘FIGC’ Gabriele Gravina ametoa taarifa ya kusikitishwa na kifo cha Vialli kwa kusema, Gwiji huyo alikuwa mtu imara na madhubuti katika mchezo wa Soka na ataendelea kukumbukwa.

“Gianluca alikuwa mtu mzuri na anaacha pengo ambalo haliwezi kuzibika,”

“Nilitumaini hadi mwisho kwamba angeweza kufanya muujiza mwingine. Hata hivyo nimefarijiwa na uhakika kwamba alichofanya kwenye Soka la Italia na hatasahaulika kamwe.” amesema Gabriele Gravina

Wakati huo huo ‘FIGC’ imetoa taarifa za kuomboleza kifo cha Vialli, na Wachezaji wote watapata wasaa wa kumkumbuka na kumuombea kwa Dakika Moja kabla ya michezo yote itakayochezwa mwishoni mwa juma hili.

Robertinho: Sina la kusema Simba SC
Washangaa uporaji wa haki za Wanawake