Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo Machi 29, 2022, imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
Kamati hiyo imepitisha makadirio hayo baada ya awali kupokea taarifa za utekelezaji wa bajeti ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Februari 2022.
Aidha kamati ilionyesha kuridhishwa na mwenendo mzuri wa makusanyo ya wizara, maendeleo ya Sekta ya Madini, kasi ya ukuaji wa sekta pamoja na utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali inayosimamiwa na wizara na taasisi zake.
Akizungumza katika Kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dunstan Kitandula ameisisitiza wizara kuangalia namna bora itayowezesha usimamizi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na kampuni kubwa zinazofanya shughuli za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kwamba, fedha hizo zinaleta tija katika maeneo yanayozunguka migodi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameihakikishia kamati kulifanyia kazi suala hilo na kutumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa kamati hiyo walioko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka katika maeneo ambayo yanafanya vizuri katika matumizi ya fedha hizo.
Aidha, Dkt. Biteko ameishukuru kamati hiyo kutokana na ushauri inaoipatia Wizara ambao umewezesha wizara kujisahihisha na kujipima namna inavyosimamia na kutekeleza Sera na Sheria.