Kamati ya Maadili ya TFF ilIyokutana Februari 3, 2018 na Februari 17,2018, katika ofisi za TFF Karume,Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa pia ilipitia na kutoa hukumu ya tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi na kughushi leseni za usajili zilizowakabili watuhumiwa mbalimbali walioletwa mbele yake.
Tuhuma hizo zilitokana na mechi namba 26 kundi A Ligi Daraja la Kwanza iliyofanyika 29 Oktoba 2017 kati ya Mvuvumwa FC na Friends Rangers ambapo katika mchezo huo timu ya Mvuvumwa FC iliwachezesha wachezaji watano (5) ambao ni Elias Costa Elias (aliyevaa jezi namba 5), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (jezi namba 7), Dunia Abdala Dunia (jezi namba 1), Doto Justine Kana (jezi namba 12) na Mwarami Abdala Mwarami (jezi namba 8).
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliwafungulia mashtaka watuhumiwa
- Dr. Yared Fubusa – Mwenyekiti na Mmiliki wa timu ya Mvuvumwa FC
- Ramadhani Kimilomilo – Katibu wa Mvuvumwa FC
- Joseph Kanakamfumu – Kocha na Mratibu wa Mvuvumwa FC
- Elias Costa Elias – Mchezaji wa Mvuvumwa FC
- Lukwesa Joseph Kanakamfumu – Mchezaji wa Mvuvumwa FC
- Dunia Abdala Dunia – Mchezaji wa Mvuvumwa FC
- Doto Justine Kana – Mchezaji wa Mvuvumwa FC
- Mwarami Abdala Mwarami – Mchezaji wa Mvuvumwa FC
- Yusuph Makoya – aliyekuwa mratibu wa mwanzo wa Mvuvumwa FC na mmiliki wa nyumba ambayo timu hiyo ilipanga kwa ajili ya kuweka kambi jijini Dar es Salaam.
TUHUMA ZILIZOWASILISHWA
Watuhumiwa 4 (Dr. Yared Fubusa, Ramadhani Kimilomilo, Joseph Kanakamfumu, na Yusuph Makoya) ambao ni viongozi wa Mvuvumwa FC walishtakiwa kila mmoja kwa makosa mawili;
- Kutoa taarifa zisizo sahihi/udanganyifu ili kufanikisha usajili wa wachezaji kinyume na kifungu cha 41(12) ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza toleo la 2017. Kama ilivyo ainishwa kwenye Kanuni za Maadili Toleo la 2013 kifungu cha 5.
- Kugushi leseni kipindi cha usajili kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Watuhumiwa 5 (Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdala Dunia, Doto Justine Kana, Mwarami Abdala Mwarami) ambao ni wachezaji wa Mvuvumwa FC
- Kushiriki mechi namba 26 kundi A Ligi daraja la kwanza iliyofanyika 29 Oktoba 2017 kati ya Mvuvumwa FC na Friends Rangers, huku wakijua usajili wao haujakamilika ikiwa ni kinyume na kifungu 37(14) cha Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza toleo la 2017.
-
Udanganyifu na kugushi leseni wakati wa usajili kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
MAHOJIANO NA WATUHUMIWA
Kamati ilifanya mahojiano na watuhumiwa Ramadhani Kimilomilo, Joseph Kanakamfumu, Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu na Yusuph Makoya. Wachezaji Dunia Abdala Dunia, Doto Justine Kana, na Mwarami Abdala Mwarami walishindwa kufika wa sababu mbalimbali huku Dr. Yared Fubusa akigoma kuja kuhojiwa na Kamati.
Katika mahojiano hayo Kamati ilibaini mambo yafuatayo;
- Uendeshaji wa timu ya Mvuvumwa FC umekuwa usioridhisha hasa baada ya kuhamisha michezo yake ya Ligi Daraja la Kwanza kutoka kituo cha Kigoma na kuja Dar es Salaam. Licha ya kuhamishia makazi yake Dar es Salaam, viongozi wakuu waliendelea kubaki Kigoma na hivyo timu kuonekana kama imetelekezwa. Majukumu ya timu alikabidhiwa Ndugu Idd Thabiti ambaye katika taarifa ya mwamuzi wa Mechi Na. 26 aliorodheshwa kama Meneja (Team Manager). Ndugu Idd Thabit, anayejulikana kwa jina maarufu “Omba” ndiye alikuwa mratibu wa timu ikiwa Dar es Salaam. Hata hivyo hakuna taarifa zozote zilizowasilishwa mbele ya Kamati kuonyesha kama “Omba” alitambulishwa kama mmoja wa viongozi wa Mvuvumwa FC.
Baadaye Uongozi wa Mvuvumwa FC ulimteua Ndugu Joseph Kanakamfumu kuwa kocha na mratibu wa timu kupitia barua pepe (email) ya tarehe 12 Oktoba 2017, na kama ilivyothibitishwa na Ndugu Ramadhani Kimilomilo Katibu wa Mvuvumwa FC alipohojiwa na Kamati. Hata hivyo Kamati haikuonyeshwa nyaraka zozote kuthibitisha makabidhiano ya timu kati ya Ndg. Joseph Kanakamfumu na “Omba” aliyekuwa mratibu kabla yake. Aidha Kamati ilithibitishiwa na Ndg. Kimilomilo kuwa hakuna mkataba wowote kati ya Ndg. Joseph Kanakamfumu na Mvuvumwa FC unaoinisha haki na majukumu ya kila upande. Mazingira kama haya yanatoa mwanya wa kutowajibika kwa pande zote.
Kutokana na kukosekana kwa mfumo unaozingatia taratibu, viongozi wake (Dr. Yared Fubusa – Mwenyekiti na Mmiliki; Ndg. Kimilomilo – Katibu; na Ndg. Kanakamfumu – Kocha na Mratibu) waliendelea kuendesha timu kiholela. Kutokana na kutozingatiwa kwa taratibu, sasa hivi kuna mgogoro kati ya Ndg. Yusuph Makoya, mmiliki wa nyumba ambayo Mvuvumwa FC iliweka kambi mara baada ya kuhamishia michezo yake kituo cha Dar es Salaam. Ndg. Makoya, ambaye aliieleza Kamati kwamba alikuwa anasaidiana na viongozi kuendesha timu, aliingia mkataba wa kuipangisha Mvuvumwa FC kwenye nyumba yake iliyopo nguvu kazi ( Chanika )kwa kipindi cha Miezi 6.Hata hivyo timu hiyo ilihamishwa kinyemela bila yeye kutaarifiwa wala kulipwa madai yake na kusababisha upotevu/uharibifu wa mali zake. Suala hili limefikishwa katika vyombo vya dola.
- Uhamishaji wa timu ya Mvuvumwa kutoka kituo cha Kigoma kuja Dar es Salaam haukuwa na uwazi wala kufuata taratibu zinazotakiwa. Alipoulizwa sababu za kuhamishia timu Dar es Salaam badala ya Kigoma ilikosajiliwa Ndg. Kimilomilo alisema kuwa timu yao inapigwa vita kule Kigoma. Kitendo cha kuhamishia timu Dar es Salaam bila kuzingatia taratibu ndicho kilisababisha iendeshwe kiholela na kuwapa mwanya wa kufanya mambo kienyeji ikiwamo kugushi leseni za wachezaji.
- Usajili wa wachezaji watano wa Mvuvumwa FC, ambao ni Elias Costa Elias (leseni namba 51992), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (leseni namba 51995), Dunia Abdala Dunia (leseni namba 51994), Doto Justine Kana (leseni namba 51997), na Mwarami Abdala Mwarami (leseni namba 51995) haukuwa halali; hakuna rekodi yoyote ya leseni hizo TFF. Hivyo wachezaji hao walishiriki Mechi Na. 26 isivyo halali.
Wachezaji hao walisajiliwa katika kipindi cha dirisha dogo na kupewa leseni zilizotolewa tarehe 28 Desemba 2017 zenye namba: Elias Costa Elias (950307002), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (980509002), Dunia Abdala Dunia (970625006), Doto Justine Kana (970417002), na Mwarami Abdala Mwarami (970914003). Huu ni uthibitisho kuwa kulikuwa na udanganyifu kwa vile mchezaji hawezi kusajiliwa mara mbili ndani ya msimu mmoja kwa timu ile ile.
- Taarifa ya mwamuzi wa Mechi Na. 26 inaonyesha kuwa namba ya leseni za wachezaji Lukwesa Joseph Kanakamfumu (aliyevaa jezi namba 7) na Mwarami Abdala Mwarami (jezi namba 8) ilikuwa na moja: 51995. Katika mazingira ya kawaida namba za leseni za usajili wa wachezaji wawili haziwezi kufanana kwa tarakimu zote.
- Ndg. Joseph Kanakamfumu aliieleza Kamati kuwa wakati anakabidhiwa timu na “Omba” aliikuta ikiwa na wachezaji wachache. Hata hivyo wakati anakabidhiwa timu anasema kuwa alipokea kadi za wachezaji hao watano ingawa hawakuwepo kambini. Wachezaji waliofika mbele ya Kamati (Elias Costa Elias na Lukwesa Joseph Kanakamfumu) waliithibitishia Kamati kuwa hawakukamilisha usajili baada ya kutolipwa fedha za usajili. Alipoombwa kutoa uthibitisho wa kupokea kadi za wachezaji hao watano kutoka kwa “Omba”, Ndg. Joseph Kanakamfumu hakuweza kutoa nyaraka zozote kuonyesha makabidhiano hayo. Aidha alipoulizwa na Kamati kwanini hakutaka kujiridhisha kama wachezaji hao wamesajiliwa kwa kuangalia kumbukumbu zilizoko TFF hakuweza kutoa majibu yoyote.
- Kwa mujibu wa maelezo ya Ndg. Kimilomilo, wachezaji hao watano hawakuwemo katika orodha aliyokabidhiwa Ndg. Joseph Kanakamfumu, hivyo hawakupaswa kuwemo katika orodha ya timu wala kushiriki Mechi Na. 26 kwa vile walitakiwa kusajiliwa kipindi cha dirisha dogo. Kamati ilipata uthibitisho kuwa wachezaji hao wanatoka katika Kituo cha Mpira wa Miguu (Football Academy) inayoendeshwa na Ndg. Joseph Kanakamfumu; hivyo ni wazi kuwa alikuwa anafahamu kila kilichokuwa kinaendelea.
- Kuna uwezekano wa udanganyifu kufanyika ndani ya mfumo wa usajili pale inapotokea baadhi ya maafisa wa TFF wasiokuwa na uaminifu kushirikiana na viongozi wa vilabu. Kwenye maelezo ya baadhi ya watuhumiwa ilionekana kuwa usajili wa Mvuvumwa FC ulifanywa kwa kiasi kikubwa na mfanyakazi wa TFF aliyejulikana kwa jina la Michael. Kamati ilipofuatilia ilielezwa kuwa mtumishi huyo aliondolewa na uongozi mpya wa TFF.
HUKUMU
- Wachezaji Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdala Dunia, Doto Justine Kana, na Mwarami Abdala Mwarami
Kamati haikuwakuta na hatia yoyote wachezaji hawa kwa vile walishiriki Mechi Na. 26 baada ya kupotoshwa na viongozi wao kwa kuaminishwa kuwa usajili wao ulikamilika na wakapewa sehemu ya fedha walizoahidiwa kwa ajili ya kusaini. Vile vile wachezaji hawa hawahusiki na suala la usajili, hivyo hakukuwa na uwezekano wa wao kugushi leseni.
Hata hivyo Kamati inawakumbusha wachezaji wote kuwa makini wakati wa kufanya makubaliano na timu zao kwani mpira ni ajira kwao. Suala kama hili linaweza kuwanyima fursa ya kukitumikia kipaji chao na kuwasababishia matatizo ambayo yanaweza kuepukwa kwa wao kuwa makini. Endapo wanakutana na vikwazo au kuhisi mazingira ya ubabaishaji ni vizuri waombe ushauri na msaada TFF.
- Ndg. Joseph Kanakamfumu – Kocha na Mratibu wa Mvuvumwa FC
Kamati imemtia hatiani kwa makosa yote mawili; Kutoa taarifa zisizo sahihi/udanganyifu ili kufanikisha usajili wa wachezaji kinyume na kifungu cha 41(12) ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza toleo la 2017 na kugushi leseni kipindi cha usajili kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Katika kosa la kwanza, Ndg. Kanakamfumu, akiwa kocha wa Mvuvumwa FC aliwaorodhesha wachezaji Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdala Dunia, Doto Justine Kana, na Mwarami Abdala Mwarami kushiriki Mechi Na. 26 huku akijua kuwa hawana leseni halali kutoka TFF. Wachezaji wote hao walitoka katika kituo (academy) anayoiendesha, hivyo ni dhahiri kuwa alijua alichokuwa anafanya.
Katika kosa la pili, Ndg. Kanakamfumu aliamua kuwaongeza wachezaji hao baada ya kukabidhiwa timu kwa vile alifahamu uwezo wao na inaonekana alitumia uzoefu wake katika mpira wa miguu kupata leseni hizo za kugushi.
Kwa makosa hayo, Kamati inamfungia Ndg. Joseph Kanakamfumu kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5). Adhabu hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.
- Ndg. Ramadhani Kimilomilo – Katibu wa Mvuvumwa FC
Kamati imemtia hatiani kwa kosa kushiriki kugushi leseni kipindi cha usajili kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Ndg. Kimilomilo akiwa kama Mtendaji Mkuu wa Mvuvumwa FC alishindwa kusimamia timu yake ipasavyo na kusababisha ichezeshe wachezaji wasio na leseni. Aidha Ndg. Kimilomilo hakutoa taarifa TFF wala Bodi ya Ligi au kuchukuwa hatua zozote kwa Ndg. Joseph Kanakamfumu licha ya kukiri mbele ya Kamati kuwa wachezaji hao hawakuwemo katika orodha ya Mvuvumwa FC. Hii inamaanisha kuwa alishirikiana na viongozi wenzake kugushi leseni ili kuiongezea nguvu timu yake.
Kwa makosa hayo, Kamati inamfungia Ndg. Ramadhani Kimilomilo kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5). Adhabu hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.
- Dr. Yared Fubusa – Mwenyekiti na Mmiliki wa Mvuvumwa FC
Kamati imemtia hatiani kwa kosa la kushiriki kugushi leseni kipindi cha usajili kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Dr. Yared Fubusa akiwa Mwenyekiti na Mmiliki wa Mvuvumwa FC amehusika kwa sehemu kubwa katika uendeshaji mbovu wa timu hali iliyosababisha matatizo mengi ikiwa suala la kugushi leseni za wachezaji Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdala Dunia, Doto Justine Kana, na Mwarami Abdala Mwarami Abdala Dunia, Doto Justine Kana, na Mwarami Abdala Mwarami.
Kwa mujibu wa maelezo ya Ndg. Joseph Kanakamfumu, kulikuwa na mawasiliano kati yake na Dr. Fubusa kuhusiana na uendeshaji wa timu. Hata suala la kuongeza wachezaji ili kuimarisha timu liliwezekana baada ya kupatikana fedha za kuwalipa kwa ajili ya kupata saini zao. Maelezo hayo yalithibitishwa na Ndg. Kimilomilo, Katibu wa Mvuvumwa FC. Kamati inaona kuwa Dr. Fubusa, ambaye alikuwa anatoa fedha za uendeshaji wa timu, alikuwa anapewa taarifa zote za matumizi yake. Aidha kama Mwenyekiti na Mmiliki alipaswa kujua kila kinachoendelea katika timu yake.
Alipopewa taarifa ya wito wa kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Dr. Fubusa alinukuliwa akisema kwa njia ya simu kuwa “TFF ni wapumbavu, mimi siwezi kuja huko. Kwanza mimi ndiyo mhanga”. Kauli hiyo ni ya dharau na ni kinyume na Kifungu cha 73(5) & (8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Kwa makosa hayo, Kamati inampa adhabu zifuatazo;
- Kwa kosa la kukaidi wito huku yeye akiwa mwanafamilia ya mpira wa miguu, Kamati inamfungia kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja na faini ya shilingi milioni tatu (Sh.3,000,000.00). adhabu hii ni kwa mujibu wa 73(5) & (8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
- Kwa kosa la kusaidia kugushi leseni za wachezaji wa Mvuvumwa FC ili washiriki Mechi Na. 26, Kamati inamfungia kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5). Adhabu hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.
Adhabu zote mbili atazitumikia kwa pamoja